Zari awaeleza wanawe sifa za wanawake anaotaka wachumbiane nao, awaonya dhidi ya ushoga

Zari aliwashauri wanawe kuchumbiana na wasichana wengi, na kuwaonya dhidi ya kuchumbiana na wanaume wenzao.

Muhtasari

•Mama huyo wa watoto watano alisikika akiwashinikiza wanawe wachumbiane na wasichana wengi wanavyotaka.

•Mama huyo wa watoto watano hata hivyo aliwapa wanawe sifa maalum ambazo anataka rafiki zao kike wawe nazo.

Zari na wanawe Pinto Tale na Raphael Tale
Image: INSTAGRAM// ZARI HASSAN

Mwanasosholaiti na mfanyibiashara maarufu wa Uganda Zari Hassan alikuwa na mazungumzo nyeti kuhusu mahusiano na wanawe Quincy na Raphael Ssemwanga.

Katika video alizoshiriki kwenye akaunti yake ya Instagram, mama huyo wa watoto watano alisikika akiwashinikiza wanawe wachumbiane na wasichana wengi wanavyotaka.

Zari alianza mazungumzo baada ya mtoto wake Raphael kumjulisha kwamba alikuwa akienda kukutana na marafiki zake.

"Niambie ukweli, utakutana na wasichana, sindio? Unajua tunaweza kuongea kuhusu haya mambo..” Zari alimwambia mwanae Quincy.

Quincy hata hivyo alikana kuwahi kuwa na mpango wa kukutana na wasichana, jambo ambalo lilionekana kumshtua sana mama yake.

Mwanasosholaiti huyo alitumia fursa hiyo kumshauri mwanawe kuchumbiana na wasichana, na kumuonya dhidi ya kuchumbiana na wanaume wenzake.

"Napenda kukusikia ukisema utakula na wasichana, kuliko marafiki. Unajua kizazi hiki kimeharibika, tunataka kukuona ukitoka na wasichana. Sijali nyinyi watu kuchumbiana na wasichana,” Zari alimwambia mwanawe.

Mwanawe mwingine, Raphael alifichua kwamba Quincy alikuwa akienda kukutana na wasichana, jambo ambalo lilionekana kuleta utulivu kwa mwanasosholaiti huyo.

“Nimefurahi, nenda ukawaone wasichana. Ni nzuri. Ninawapenda nyinyi watu kwa hilo, kwa sababu jambo linalofuata, nitashtuka nikigundua mtu anachumbiana na mvulana mwenzake. Nenda ukawaone wasichana, wengi kadiri unavyotaka. Nina furaha kuhusu hilo. Niko sawa nayo,” alisema.

Mama huyo wa watoto watano hata hivyo aliwapa wanawe sifa maalum ambazo anataka rafiki zao kike wawe nazo.

"Hakikisha wanapendeza kama mimi, watazeeka kama mimi, warembo kama mimi, wenye akili kama mimi, wachapa kazi kama mimi," aliwaambia wanawe kabla ya kukatishwa na bintiye Tiffah Dangote.

Huku akimgeukia mwanawe mwingine Raphael, mzazi-mwenza huyo wa staa wa bongo Diamond Platnumz alikosoa mtindo wake wa mavazi akisema anaonekana shoga. Alimfanya abadilishe nguo zake kabla ya kuondoka kwenda kuonana na wasichana.