Nadia Mukami amsakama Ezekiel Mutua kwenye koo kisa mirabaha yake ya MCSK tangu 2017

Nadia alijitokeza kudai haki saa chache baada ya MCSK chini ya uongozi wa Ezekiel Mutua kushindwa kueleza kinagaubaga zilipo milioni 56 zilizokusanywa kutokana na kazi za wasanii mwaka wa 2023.

Muhtasari

• Ni kinaya kwamba msanii huyo hajawahi pokea mapato yake ya mirabaha kutokana na kazi zake ambazo zimeenea pakubwa mpaka kumzolea tuzo ya AFRIMMA.

Nadia na Mutua
Nadia na Mutua
Image: Facebook

Msanii wa muziki wa Pop kutoka humu nchini Nadia Mukami amejitokeza kuituhumu taasisi inayosimamia hakimiliki za kazi za Sanaa nchini MCSK kwa kutompa mirabaha yake tangu mwaka 2017.

Nadia alijitokeza katika mitandao ya kijamii saa chache baada ya MCSK chini ya uongozi wa Dkt Ezekiel Mutua kushindwa kueleza kinagaubaga zilipo milioni 56 zilizokusanywa kutokana na kazi za wasanii katika mwaka wa 2023.

Akieleza kusikitishwa kwake, Mukami alisema kwamba tangu 2017 alipojiandikisha rasmi kama mwanachama wa MCSK kama msanii mpya, ajabu ni kwamba hajawahi  pokea hata shilingi moja licha ya kazi zake za Sanaa kuwa maarufu ndani na nje ya nchi.

“Sijawahi pokea pesa zozote za MCKS, licha ya kwamba nilijisajili kama mwanachama mwaka 2017 nikiwa msanii mpya. Mbona mimi MCSK?” Mukami aliuliza kupitia instastory yake.

Ni kinaya kwamba msanii huyo hajawahi pokea mapato yake ya mirabaha kutokana na kazi zake ambazo zimeenea pakubwa mpaka kumzolea tuzo ya AFRIMMA katika kitengo cha msanii bora wa kike ukanda wa Afrika Mashariki mwaka 2023.

Baada ya Ezekiel Mutua na timu yake katika MCSK kushindwa kueleza zilizo pesa hizo milioni 56 kutoka kwa maokoto ya kazi za Sanaa mwaka 2023, Kesi hiyo imekabidhiwa kwa Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC) na Mkurugenzi wa Uchunguzi wa Jinai (DCI) kwa uchunguzi.