Willy Paul afafanua kwa nini hakukolabo na msanii yeyote wa Kenya kwenye albamu yake mpya

Idadi kubwa ya ngoma hizo ni kolabo na wasanii wa Bongo Fleva kutoka Tanzania na Afrobeats kutoka Nigeria.

Muhtasari

• Kando na ngoma zake binafsi kama Umeme, My child my love na Isabella, Willy Paul pia ameshirikiana na wasanii wa Bongo akiwemo Marioo, Nandy.

 
• Pia kuna kolabo na wasanii wa Afrobeats kama Iyanya, Guchi, miongoni mwa wengine

WILLY PAUL
WILLY PAUL
Image: Instagram

Willy Paul, msanii wa kizazi kipya humu nchini anatarajia kuachia albamu yake kesho Jumanne Aprili 30.

Albamu hiyo aliyoipa jina ‘Beyond Gifted’ ina jumla ya nyimbo 14, nyingi yazo zikiwa ni kolabo na wasanii mbalimbali.

Hata hivyo, wenye jicho la mwewe katika udadisi waligundua kwamba katika ngoma zote hizo haswa kolabo, hakuna wimbo hata mmoja ambao Pozee amemshirikisha msanii hata mmoja kutoka humu nchini licha ya kuwa yeye ni msanii wa Kenya.

Idadi kubwa ya ngoma hizo ni kolabo na wasanii wa Bongo Fleva kutoka Tanzania na Afrobeats kutoka Nigeria.

Baada ya maswali mengi kuibuliwa, Willy Paul kupitia Instastory yake alirejea na kutoa majibu kwa kufafanua sababu ya kutowashirikisha wasanii wa Kenya kwenye albamu hiyo mpya.

Kwa mujibu wa Willy Paul, wasanii wengi wa Kenya wana ubinafsi na roho mbaya ndicho kitu tu ambacho wengi wao wanamudu tena kwa bei nafuu, hivyo aliamua kuwaweka pembeni.

“Nimeona maswali mengi kuhusu ni kwa nini hakuna msanii hata mmoja wa Kenya kwenye albamu yangu. Kwani mumesahau kuwa wasanii wengi wa Kenya roho mbaya tu ndicho kitu wanamudu kwa bei nafuu? Albamu inatoka kesho mapema,” Willy Paul alisema.

Kando na ngoma zake binafsi kama Umeme, My child my love na Isabella, Willy Paul pia ameshirikiana na wasanii wa Bongo akiwemo Marioo, Nandy.

Pia kuna kolabo na wasanii wa Afrobeats kama Iyanya, Guchi, miongoni mwa wengine.