Kiongozi wa upinzani Raila Odinga amevunja kimya chake kuhusu mgomo wa madaktari kwa kuitaka serikali ishughulikie matakwa yao ili warejee kazini.
Waziri huyo mkuu wa zamani alisema raia maskini wasioweza kumudu gharama ya huduma za matibabu katika hospitali za kibinafsi ndio wanaumia baada ya mgomo huo kuathiri huduma katika hospitali za umma.
“Hali inaendelea kuwa mbaya na hivi karibuni, huenda tukashuhudia janga kubwa baada wahudumu wote kususia kazi. Tayari maafisa wa kliniki wamejiunga na mgomo huo,” Odinga amesema.
“Kwa hivyo, serikali ikutane na madaktari, wajadiliane kuhusu masuala yaliyoibuliwa ili kukomesha mateso kwa Wakenya,” akaongeza.
Odinga alisema hayo kwenye kikao na wanahabari jijini Nairobi huku mgomo wa madaktari ukiingia wiki yake ya nne.
Pia aliangazia udumishaji wa mishahara ya wahudumu wa afya katika Ksh.206,000 kama ilivyoainishwa katika Mkataba wa Makubaliano ya Pamoja (CBA) uliotiwa saini 2017 kama mojawapo ya njia zitakazosuluhisha mzozo huo, kabla ya makubaliano mapya kuafikiwa.