Sehemu ya barabara ya UN kuelekea Runda yafungwa na KURA kutokana na mafuriko

Barabara hiyo imefungwa kutokana na kuendelea kuongezeka kwa kina cha maji katika barabara hiyo.

Muhtasari

•Kura imetangaza kufunga sehemu ya barabara ya Umoja wa Mataifa ya Runda kutokana na mafuriko.

•Mamlaka iliwataka madereva kutumia njia mbadala kuelekea wanakoenda.

Sehemu iliyojaa mafuriko ya barabara ya United Nations Avenue
Image: Hisani

Mamlaka ya Barabara za Mijini nchini (Kura) imetangaza kufunga sehemu ya barabara ya Umoja wa Mataifa ya Runda kutokana na mafuriko.

Katika taarifa yake Jumatatu, Mamlaka hiyo ilisema barabara hiyo imefungwa kutokana na kuendelea kuongezeka kwa kina cha maji katika barabara hiyo.

Ilisema haya ni matokeo ya mvua kubwa iliyonyesha Jumapili usiku.

“Mamlaka ya Barabara za Mijini ya Kenya inasikitika kufahamisha umma kwamba UN-Avenue, Runda imefungwa kutokana na maji kupanda barabarani kufuatia mvua kubwa iliyonyesha jana usiku.

"Sehemu zilizoathiriwa ni kati ya mzunguko wa Barabara ya Ruaka na Magnolia karibu. (Mkahawa wa Lord Erroll)." sehemu ya taarifa hio ilisema.

Mamlaka imewataka madereva kutumia njia mbadala za kuelekea wanakoenda.

Kura aliongeza kuwa wataendelea kufuatilia hali ilivyo.

"Tunafuatilia kwa karibu hali ilivyo na tutatoa taarifa kuhusu maendeleo. Tunawaomba madereva kutumia njia mbadala na kuchukua tahadhari."

Mvua kubwa inayoendelea kunyesha jijini Nairobi na kote nchini imesababisha uharibifu mkubwa wa mali pamoja na kupoteza maisha.

Hii pia imeshuhudia kufungwa kwa barabara, miongoni mwa hatua zingine zinazochukuliwa na serikali kuwaweka Wakenya salama.

Watu wamehimizwa kuhamia maeneo ya juu na salama kutokana na mafuriko nyumbani.