Chakula cha wanafunzi chagawa kwa watu baada ya wizara kusitisha shule kufunguliwa

" Mpango wetu ulikuwa kupikia wanafunzi 10,650 na hivyo maandalizi yalianza saa kumi jioni jana na kupika kulianza saa nane na baadae tukapokea ujumbe wa kutofunguliwa kwa shule" mpishi alisema.

Muhtasari

• Maandalizi ya chakula hicho yalikuwa yameanza jana usiku kabla ya kutolewa kwa waraka wa Wizara ya Elimu wa kufuta tarehe ya ufunguzi wa Jumatatu.

Chakula cha shule
Chakula cha shule
Image: screengrab

Wakaazi wa eneo bunge la Limuru huko Kiambu leo ​​walipokea chakula cha mchana bila malipo kwa hisani ya mpango wa kulisha shuleni baada ya serikali kusukuma tarehe za kufunguliwa hadi Mei 6.

Viongozi katika jiko kuu la Kamandura, ambalo huandaa chakula cha mchana kwa zaidi ya wanafunzi elfu kumi kote Limuru, ilibidi wagawie chakula hicho kwa wakaazi na familia zilizo hatarini katika eneo hilo ili kuepusha ufujaji.

Maandalizi ya chakula hicho yalikuwa yameanza jana usiku kabla ya kutolewa kwa waraka wa Wizara ya Elimu wa kufuta tarehe ya ufunguzi wa Jumatatu.

Hata hivyo wazazi wameitupia lawama Serikali kwa kutoa agizo hilo ghafla na kuomba maagizo hayo yatolewe kwa wakati ili kuepusha usumbufu huo.

Wanafunzi wa shule ya msingi Kamandura waliokuwa wameripoti katika taasisi hiyo walilazimika kurejea majumbani mwao.

Mpishi alisema kwamba kufikia jana, walikuwa wameandaa chakula na uamuzi wa usiku wa manane kutoka kwa waziri wa elimu Ezekiel Machogu kusitisha kufunguliwa kwa shule kwa wiki moja Zaidi kuliwapelekea kusalia na chakula bila walaji.

“Kufikia jana, tulikuwa tayari tumeanza kutayarisha chakula kwa ajili ya watoto. Mpango wetu ulikuwa kupikia wanafunzi 10,650 na hivyo maandalizi yalianza saa kumi jioni jana na kupika kulianza saa nane na baada ya kupokea ujumbe wa kutofunguliwa kwa shule, tulianza kutathmini pahali pa kupeleka chakula,” mpishi alisema.

“Tulipeleka chakula hicho kwa familia zenye uhitaji katika mitaa ya mabanda ya Gishagi na Limuru Mission Primary,” aliongeza.

Tazama video jinsi wakaazi hao walipokea chakula cha bure.