Hisia mseto baada ya serikali kuahirisha ufunguzi wa shule usiku wa manane

Baadhi ya Wakenya wamekosoa uamuzi wa serikali wa kuahirisha ufunguzi wa shule dakika za mwisho.

Muhtasari

•Wizara ya elimu ilitoa taarifa usiku wa kuamkia Jumatatu ikitangaza kuwa shule za msingi na za upili hazitafunguliwa Aprili 29.

•Kufuatia taarifa hiyo ya serikali, Wakenya wamejitosa kwenye mitandao mbalimbali ya kijamii kutoa maoni yao kuhusiana na hatua hiyo.

ya watoto wakielekea shuleni.
Picha ya maktaba ya watoto wakielekea shuleni.
Image: MAKTABA

Wakenya wameeleza hisia mseto baada ya serikali kufanya uamuzi wa dakika za mwisho wa kuahirisha kufunguliwa kwa shule kwa muhula wa pili wa mwaka wa masomo 2024.

Wizara ya elimu ilitoa taarifa usiku wa kuamkia Jumatatu ikitangaza kuwa shule za msingi na za upili hazitafunguliwa Aprili 29, kama ilivyokuwa imeratibiwa hapo awali.

Waziri wa Elimu Ezekiel Machogu alisema wamepokea data kuwa baadhi ya shule zimeathiriwa vibaya na mafuriko yanayoendelea na hivyo akasema shule zifunguliwe wiki ijayo.

Alisema kuwapeleka wanafunzi na wafanyikazi katika shule zilizoathiriwa itakuwa kuweka maisha yao hatarini, kwa hivyo uamuzi wa kuahirisha kufunguliwa tena.

"Athari mbaya za mvua katika baadhi ya shule ni kubwa sana hivi kwamba haitakuwa jambo la busara kuhatarisha maisha ya wanafunzi na wafanyikazi kabla ya hatua za kuzuia maji kuchukuliwa ili kuhakikisha usalama wa kutosha wa jamii zote za shule zilizoathiriwa.

“Kutokana na tathmini hii, Wizara ya Elimu imeazimia kuahirisha kufunguliwa kwa shule zote za msingi na sekondari kwa wiki moja hadi Jumatatu, Mei 6, 2024,” Machogu alisema.

Shule zilipangwa kufunguliwa tena  leo Jumatatu, Aprili 29 .

Waziri Machogu alisema Wizara yake itashirikiana na mashirika na wadau husika kuweka mikakati ya kukabiliana na athari za mvua.

Aliongeza kuwa pia watatoa taarifa za mara kwa mara kuhusu maendeleo yote yanayohusu sekta ya elimu.

Kufuatia taarifa hiyo ya serikali, Wakenya wamejitosa kwenye mitandao mbalimbali ya kijamii kutoa maoni yao kuhusiana na hatua hiyo.

Baadhi ya wanamitandao wamekosoa uamuzi wa serikali wa dakika za mwisho,  wengine wakipongeza hatua hiyo huku wengine wakikejeli taarifa hiyo kutokana na muda ilipotolewa.

Tazama maoni ya baadhi ya Wakenya kwenye mtandao wa Twitter:-

Henry Kabogo: Asante! Lakini kwa kweli,, hatungehatarisha maisha ya watoto wetu kwa njia yoyote ile.

Kachwanya: Kwa nini uamuzi huu wa wazi haukufanywa mapema, baadhi ya watoto tayari wako njiani kuelekea shuleni kwao.

Ongeri: The super CS hatimaye amefanya uamuzi wa busara.

Felix Makinda: Kutoa notisi kwa umma saa saba unusu usiku, hii inakusudiwa wachawi sio wazazi. Wazazi walilala saa moja usiku.

Griffins Osiemo Ongori: Kwa nini msitumie data kutoka kwa idara ya utabiri wa hali ya anga kutoa taarifa kwa wakati! Walisema mvua itanyesha kwa siku 4 nyingine, haukuhitaji kungoja hadi Jumatatu kufanya uamuzi huo kuwa marufuku!

Mwalimu Kabetes Kibet: Hatua nzuri lakini kwa nini CS itoe habari kama hizi hadi sasa?