Kiambu: Katoliki yaruhusu mume kufunga harusi na mke wa kwanza mke, wa pili akitazama tu!

“Hawakubali kuweka pete watu wawili mbele ya kanisa, lakini tukiwa nje mimi nitatangaza na nionyeshe dunia kuwa hawa ni wanawake wangu na ninawapenda kwa viwango sawa,” Mzee huyo alisema.

Muhtasari

• Ndacu alifunga ndoa na mkewe wa kwanza ambaye walioana kwa Zaidi ya miaka 40 iliyopita, Margret Nyokabi.

Mume afunga arusi na mke wa kwanza, wa pili akitazama.
Mume afunga arusi na mke wa kwanza, wa pili akitazama.
Image: Screengrab

Shangwe na mbwembwe zilishuhudiwa katika kanisa moja la Kikatoliki kaunti ya Kiambu baada ya mume mwenye wake wawili kuruhusiwa na kanisa kufunga harusi na mke wa kwanza huku mke wa pili akifuatilia kama shuhuda.

Katika kile kilichovutia maoni ya wengi, harusi hiyo isiyo ya kawaida baina ya Patrick Ndacu na mke wake wa kwanza ilifanyika katika kanisa la Kikatoliki kaunti ya Kiambu.

 Kwa mujibu wa ripoti ya harusi hiyo ambayo iliangaziwa kwenye runinga ya Citizen, Ndacu aliandika wosia wa kugawa urithi wake pasu kwa pasu baina ya wake zake wawili kabla ya kupata kibali cha kufunga harusi.

Kanisa hilo lilisema kwamba iliwachukua muda wa takriban miaka 5 ili kufikia uamuzi wa kumruhusu Ndacu kufunga harusi na mke wa kwanza, huku mke wa pili akitazama jinsi shughuli nzima ilikuwa ikiendeshwa kanisani.

Ndacu alifunga ndoa na mkewe wa kwanza ambaye walioana kwa Zaidi ya miaka 40 iliyopita, Margret Nyokabi.

Mzee huyo alisema kwamba alikuwa na hamu ya kurudi kanisani ili kuanza kupokea sakramenti na kushughulika katika ujenzi wa kanisa, jambo ambalo kwa mujibu wa taratibu za kanisa Katoliki, ni sharti mtu uwe umebatizwa na umefunga harusi.

Kanisa katoliki, sawa na madhehebu mengine ya Kikristo, hairuhusu ndoa za wake Zaidi ya mmoja kwani mmoja tu ndiye anatambulika.

“Mke wa kwanza alikuwepo, akaenda akaoa tena mke wa pili na wakapata watoto na wote, lakini sasa amerudi anataka harusi na mke wa kwanza. Na wote waliketi chini na kukubaliana achague mmoja wa kufunga harusi naye, bahati ikamuangukia mke wa kwanza,” kasisi alisema.

“Tulikuja tukaitana tukakaa chini, akanigawia mali yangu, na yule mwingine yake ndio harusi ikafanyika” mke wa pili alisema.

“Hawakubali kuweka pete watu wawili mbele ya kanisa, lakini tukiwa nje mimi nitatangaza na nionyeshe dunia kuwa hawa ni wanawake wangu na ninawapenda kwa viwango sawa,” Mzee huyo alisema.