Mshikilizi wa rekodi ya Dunia ya Marathon Kelvin Kiptum alifariki kutokana na majeraha mabaya kichwani – Johansen Oduor

Alisema alivunjika kwenye fuvu la kichwa na mbavu hali iliyoathiri mapafu yake.

Muhtasari

• Msemaji wa familia Philip Kiplagat alisema wameridhishwa na maelezo ya uchunguzi wa maiti na wataendelea na mazishi ya Kiptum.

Mwanapatholojia mkuu wa serikali Dkt Johansen Oduor akizungumza katika chumba cha maiti cha hospitali ya Eldoret. 21/02/2024.
Mwanapatholojia mkuu wa serikali Dkt Johansen Oduor akizungumza katika chumba cha maiti cha hospitali ya Eldoret. 21/02/2024.
Image: MATHEWS NDANYI

Mshikilizi wa rekodi ya dunia ya mbio za Marathon Kelvin Kiptum alifariki kutokana na majeraha mabaya kichwani kutokana na ajali iliyogharimu maisha yake. 

Mwanapatholojia mkuu wa Serikali Dkt Johansen Oduor anasema uchunguzi wa mwili wake ulibaini kuwa Kiptum alipata majeraha mabaya na kuvunjika mwilini mwake. 

Alisema alivunjika kwenye fuvu la kichwa na mbavu hali iliyoathiri mapafu yake. Oduor anasema aliitwa kufanya uchunguzi wa kifo kutokana na uvumi kuhusu kifo cha mwanariadha huyo.  Alisema majeraha hayo yalisababishwa na ajali hiyo.  

Oduor alifanyia uchunguzi wa mwili wa Kiptum katika chumba cha maiti cha hospitali ya Eldoret. Uchunguzi wa maiti ulifanyika mbele ya babake Kiptum Samson Cheruiyot na maafisa wa kitengo maalum cha kuchunguza mauaji kutoka makao makuu ya DCI. 

Baada ya zoezi la uchunguzi wa maiti lililochukua zaidi ya saa mbili Dkt Oduor alifahamisha chanzo cha kifo chake kwa familia ya Kiptum kabla ya kuhutubia wanahabari. 

Oduor alisema wamechukua sampuli kutoka kwa mwili kwa uchunguzi wa sumu ili kusaidia kubaini kilichosababisha ajali hiyo. 

Msemaji wa familia Philip Kiplagat alisema wameridhishwa na maelezo ya uchunguzi wa maiti na wataendelea na mazishi ya Kiptum. "Kama familia tumeridhika na tutaendelea na maziko Ijumaa," alisema Kiplagat.

IMETAFSIRIWA NA DAVIS OJIAMBO.