Polisi katika eneo la Suba Kusini wameanzisha uchunguzi kuhusu mauaji ya mwanamke anayeripotiwa kuangamizwa na aliyekuwa mume wake kutokana na mzozo wa malezi ya watoto.
Winnie Auma, 30, alikatwa kwa panga Jumatano asubuhi katika kijiji cha Mwirendia, eneo la Kaksingri Magharibi, kabla ya mshukiwa kujisalimisha kwa polisi.
Wawili hao walitengana miaka mitatu iliyopita kutokana na mizozo ya kinyumbani.
Auma aliolewa tena kama kilomita 15 kutoka nyumba ya awali.
Kamanda wa polisi wa eneo hilo Caxton Ndunda alisema alichukua watoto wawili hadi katika nyumba yake mpya na kumwacha mshukiwa na watoto watatu.
"Tukio la mauaji lilitokea wakati wa vita wakati Auma alirudi kuchukua watoto wengine watatu kutoka kwa mume wake wa zamani," alisema.
Auma alipata majeraha kichwani na mikono yake miwili ikakatwa. Alikufa papo hapo.
Baada ya kufanya kitendo hicho cha kinyama, mtuhumiwa huyo alitembea hadi Gingo Police Post akiwa na panga lake na kuwaeleza polisi kuwa amefanya mauaji.
Ndunda alisema mtuhumiwa alikamatwa na kuzuiliwa katika kituo cha polisi, kabla ya kuhamishiwa hadi kituo cha Magunga kwa mahojiano zaidi.
Wakaazi walioshuhudia tukio hilo walisema wawili hao walikuwa na mzozo wa muda mrefu kuhusu watoto hao.
Polisi walisema wana ripoti kwamba mshukiwa aliwahi kumfukuza afisa wa watoto kutoka kaunti ndogo ya Suba, ambaye msaada wake ulikuwa umetafutwa na Auma.
Auma alitaka afisa huyo amsaidie kupata malezi ya watoto wake watatu waliosalia.
Ndunda aliwataka wanandoa kutafuta mwongozo na ushauri kuhusu masuala ya nyumbani.
"Wanandoa wanapaswa kutafuta njia zinazofaa za kushughulikia tofauti zao. Wanapaswa kukumbatia mwongozo na ushauri kutoka kwa viongozi wa dini, wazee na watu wengine ili kuzuia vitendo hivyo viovu,” alisema.
Mwili wa marehemu ulihamishiwa katika chumba cha kuhifadhi maiti cha hospitali ya kaunti ndogo ya Sindo.