Aliyekuwa gavana wa Nairobi Mike Sonko ameahidi kumpeleka Conjestina Achieng' hospitalini kwa ajili ya matibabu.
Jumamosi mwanasiasa huyo alikutana na familia ya bondia huyo wa zamani ambaye amekuwa akiugua kwa muda mrefu ili kujadili mikakati ya matibabu yake.
"Pamoja na familia ya Conjestina huku tukipanga njia ya kusonga mbele. Upande wangu wa kulia Mwanae pekee Charlton na kushoto dada Eva mwisho wao pamoja na jamaa wengine. Hata hivyo tuvumilie hatutafichua hali yake ya sasa ya kuhuzunisha," Sonko aliandika chini ya video ya mkutano wake na familia ya bondia huyo ambayo alipakia Facebook.
Katika mkutano huo, Sonko aliahidi kulipia gharama zote za hospitali za bondia huyo wa zamani hadi atakapopata nafuu.
Mgombea huyo wa ugavana wa Mombasa alisema Conjestina atalazwa katika chumba maalum ili wanafamilia na watumishi wa Mungu wanaotaka kumuombea waweze kumtembelea kwa urahisi.
"Tutakuwa naye mpaka mwisho. Haijalishi itachukua muda gani. Mradi niko hai na Mungu amenipatia uwezo nitafika mwisho na Conje," Alisema.
Sonko alifichua kuwa tayari amekutana na waziri wa michezo Amina Mohammed na kukubaliana kushirikiana katika kumsaidia Conjestina.
Pia alitoa wito kwa Wakenya wengine kujitolea kumsaidia bingwa huyo wa ndondi ambaye aliwahi kuleta utukufu nyumbani.
"Sisi tutamsadia mahali tutaweza. Familia imesema mara hii watakuwa wanamtembelea rehab. Awali alikuwa anakaa sana anaona ameachiliwa anatoroka anaenda nyumbani. Wakenya naomba tafadhali tusaidiane. Sasa anaenda hospitalini tena. Askofu yeyote, nabii yeyote ambaye anaona Mungu anasikia maombi yake aje huko," Alisema.
Mwanafamilia mmoja pia alifichua kuwa wanapanga kumpeleka Conjestina nchini Uganda kwa ajili ya maombi.
Hii sio mara ya kwanza kwa Sonko kujitolea kugharamia matibabu ya bondia huyo wa zamani ambaye amekuwa akiugua.
Hapo awalai mwanasiasa huyo amewahi kumpeleka Conjestina rehab angalau mara mbili miongoni mwa usaidizi mwingine.