Aliyekuwa gavana wa Nairobi Mike Sonko ametuma gari lake moja hadi kaunti ya Siaya kumchukua bondia wa zamani Conjestina Achieng kwa ajili ya maombi.
Kupitia taarifa yake ya Jumamosi, Sonko alidokeza kuwa familia ya bondia huyo inaamini kwamba sasa anahitaji maombi ili apate nafuu.
Mgombea huyo wa ugavana wa Mombasa amesema yupo tayari kutimiza ombi la familia ya Conjestina na kuendelea kumsaidia bingwa huyo wa ndondi ambaye hajakuwa sawa kiakili kwa muda mrefu zaidi katika kipindi cha muongo mmoja ambao umepita.
"Pamoja na kuwa na shughuli nyingi za kimahakama na dhiki nimeamua kuendelea kumsaidia ikiwa ni pamoja na kumpeleka kwa Nabi Mary Kagendo kwa ajili ya maombi. Sasa hivi natuma gari pamoja na timu yangu hadi Siaya ili kurahisisha harakati zake na pia ninaomba kwa unyenyekevu kwa yeyote anayemtakia heri na yuko tayari kusaidia tusaidiane sote kwa ajili ya huyu shujaa kwa njia zozote zile tunazoweza kupitia kwa mwana Charltone - 0724280472," Sonko alisema kupitia kurasa zake za mitandao ya kijamii.
Sonko pia amewakosoa viongozi wa Kenya kwa kutoingilia kati kumsaidia bingwa huyo wa zamani wa ndondi licha ya maombi mengi ya Wakenya na familia.
Hii sio mara ya kwanza kwa mwanasiasa huyo kujitolea kumsaidia Conjestina, hapo awali amewahi kuweka juhudi za kurejesha afya na heshima ya bondia huyo.
"Nimemsaidia peke yangu hapo awali, kumpeleka katika hospitali mbalimbali na rehab ikiwa ni pamoja na Nairobi Rehabilitation Centre iliyo Parklands, Diani Beach miongoni mwa zingine ambapo amepata afueni kamili na kuruhusiwa kuenda nyumbani kisha anaporudi kijini baada ya muda hali yake inakuwa baya tena," Sonko alisema.
Haya yanajiri siku chache tu baada ya picha za kuhuzunisha za bondia wa zamani wa kusambaa kwenye mitandao ya kijamii ambapo wanamitandao wengi waliashiria ghadhabu yao kutokana na hali yake ya sasa ya kutia huruma.
Picha hiyo ilimuonyesha Conjestina akiwa ameshikilia mlango wa gari huku mkono wa mtu asiyeonekana vizuri ukionekana kumuelekeza aingie ndani. Uso wa Achieng ulionekana bila furaha wala tabasamu kabisa.