Siku ya Ijumaa mtangazaji mkongwe wa runinga ya KBC Badi Muhsin alifariki dunia akiwa na umri wa miaka 67, familia yake ilithibitisha.
Kifo cha Badi ambacho kinaripotiwa kutokea mida ya saa kumi alasiri kilishtua Wakenya wengi ambao wameendelea kumuomboleza na kutuma risala zao za rambirambi kwa familia.
Inaripotiwa kuwa marehemualikuwa amelalamikia kuumwa na tumbo kabla ya kuenda kulala ila hakuamka tena.
Badi ambaye alianza kufanya kazi ya utangazaji katika runinga ya KBC mwaka wa 1980 alifariki akiwa mjini Mombasa ambako alikuwa ameenda kwa ziara ya kikazi.
Wakenya wengi ikiwemo watu mashuhuri na watangazaji wenzake wameendelea kumkumbuka na kumuomboleza marehemu.
Msemaji wa ikulu Kanze Dena amemhusisha marehemu na mafanikio yake kwenye ulingo wa utangazaji huku akisema kuwa kama sio kwa usaidizi wa Badi asingalikuwa mtangazaji tajika nchini.
"Kanze Dena asingelikuwa Kanze Dena kama sio wewe Badi. Uliniamini, ulinisukuma, ulinikosoa , ulinisifu hadi kifo chako. Simanya nihendedze, lakini Nashukuru saana saaana" Kanze Dena alimkumbuka Badi kupitia ukurasa wake wa Instagram.
Dena alimuita marehemu msaidizi wa hatima yake kwa kumsaidia kuwa gwiji kwenye taaluma ya utangazaji wa habari.
"Ndivyo alivyopenda Maulana hadi tutakutana tena" Aliomboleza Dena.
Dena alifichua kwamba marehemu alikuwa anamjulia hali mara kwa mara huku akisema kuwa pengo ambalo aliacha halitoweza kujazika kamwe.
"Ulikuwa unanijulia hali mara kwa mara. Tulizungumza kwa simu mara ya mwisho wakati wa uzinduzi 'Kanze Dena bado wewe timu ikamilike..' Hatukupata mda wa kukamilisha timu Badi.. Pengo lako halitajazika" Dena alimwomboleza Badi.
Mtangazaji wa Radio Jambo Gidi Ogidi amemsifia marehemu kwa kazi kubwa ambayo amefanya kwenye sekta ya utangazaji
"RIP Badi Mukhin mtangazaji mkongwe, shukran kwa mchango wako kwenye sekta ya utangazaji" Gidi alimwomboleza Badi kupitia ukurasa wake wa Instagram.