Eric Omondi ajitolea kumsaidia kupata kazi mhitimu aliyetandaza vyeti vya masomo

Eric alifichua kwamba ameweza kupata zaidi ya nafasi 400 za kazi ambazo atagawia vijana wasio na kazi.

Muhtasari
  • Masaibu ya Manyama yalivuma na kumvutia mchekeshaji Eric Omondi ambaye alitangaza kwamba atamsaidia kupata kazi.
Mcheshi Erick Omondi.
Mcheshi Erick Omondi.
Image: INSTAGRAM

Mchekeshaji Eric Omondi ameingilia kati kujitolea kumsaidia mwanamume asiye na kazi ambaye alionyesha vyeti kadhaa.

Mwanamume huyo aliyetambulika kwa jina la Alson Manyama alilalamika kuwa bado hajapata nafasi ya kuajiriwa, na kuongeza kuwa anahisi kuhuzunika na kukata tamaa.

Malalamishi yake yalivuma na kumvutia Eric, aliyejitangaza kuwa Rais wa Vichekesho barani Afrika ambaye aliapa kwamba atamsaidia kupata kazi.

Eric alifichua kuwa kwa sasa ana zaidi ya nafasi 400 za kazi ambazo atakuwa akiwapa vijana wasio na kazi huku kukiwa na tatizo kubwa la ukosefu wa ajira ambalo linawapeleka wengi kukumbwa na msongo wa mawazo.

Alitoa wito kwa yeyote anayemfahamu Manyama kuwaunganisha huku akibainisha  anataka mhitimu huyo awe miongoni mwa wanufaika wa kwanza.

"Namtafuta huyu mtu, Alson Manyama. Tumepata ajira karibu 400 na tutaanza kuzisambaza hivi karibuni nataka awe miongoni mwa wanufaika wa kwanza. Kama unamfahamu tafadhali DM namba yake au tag page yake kwenye comments, "Omondi alisema kwenye mitandao ya kijamii.

Manyama alishiriki kwamba anatarajia kuongeza unyoya mwingine kwenye kofia yake kwa kupata Shahada ya Uzamivu ya Falsafa (PhD) mwaka wa 2025.

Akiwa amevalia gauni la kuhitimu, Alson alitandaza vyeti vyake vya masomo kwenye nyasi na kupiga nao picha.

"Malengo ya 2025 = PhD. Kuwa Dk Alson Manyama. Unaweza kununua karatasi ... sio digrii," inasomeka maelezo yaliyotumika kwenye picha na vyeti vyake vya masomo.

Kulingana na wasifu wake wa Facebook, Manyama anaishi Johannesburg, Afrika Kusini.

Wasifu wake unaonyesha kuwa hivi majuzi alihitimu Shahada ya Uzamili ya Uongozi - biashara ya kidijitali kutoka Chuo Kikuu cha Wits nchini Afrika Kusini.