"Taaluma yako ilifufuliwa ikafa tena!" Davido amwambia Wiz Kid huku wakitupiana vijembe mtandaoni

Makabiliano yalianza baada ya Wizkid kuchapisha video ya Davido akidaiwa kulia huku akimbembeleza mwanamke

Muhtasari

•Davido aliandika kile kilichoonekana kuwa mashambulizi ya hila kwa mwenzake, akisema kuwa muziki wake sio maarufu tena.

•Wizkid alionekana kutupilia mbali madai ya kutofanya vizuri katika muziki, na kujigamba kuwa yeye ni bora kuliko Davido.

Wizkid na Davido
Image: HISANI

Mwimbaji maarufu wa Nigeria Ayodeji Balogun, ambaye pia anajulikana kama Wizkid, na mwenzake David Adedeji almaarufu Davido wamehusika katika vita vya maneno mtandaoni.

Vita vya maneno vilianza wikendi ambapo Wizkid, anayejulikana pia kama Starboy alichapisha  video ya Davido akidaiwa kulia huku akimbembeleza mwanamke. Video hii ilizua hisia nyingi kutoka kwa mashabiki wa waimbaji wote wawili.

Siku ya Jumatatu jioni, Davido kisha alizama kwenye Twitter ambapo aliandika kile kilichoonekana kuwa mashambulizi ya hila kwa mwenzake, akisema kuwa muziki wake sio maarufu tena.

"Hawajui gbedu [muziki] wako tena," Davido aliandika.

Wizkid alijibu, “Unajua nini, hakuna maana, jamaa wabishi, nawaombea nyote”.

Davido hata hivyo alikanusha kuwa mbishi na kumshutumu mwimbaji mwenzake kuwa 'mgonjwa'.

Wizkid alionekana kutupilia mbali madai ya kutofanya vizuri tena katika muziki, na kujigamba kuwa yeye ni bora kiimuziki kuliko Davido.

Davido aliendelea kudai kuwa taaluma ya muziki ya mpinzani wake, ilikuwa imekufa, ikafufuka kabla ya kufa tena.

"Hasa kwa nini niliacha kupoteza nguvu zangu na kuhatarisha mamilioni yangu ya dola za ridhaa kwa mtu ambaye taaluma yake ilifufuliwa miaka michache iliyopita ili kufa tena. Ifuatayo!” alisema.

Hii si mara ya kwanza kwa waimbaji hao wawili wa Nigeria kushiriki katika vita vya maneno.

Mwaka jana, Davido alidai kuwa ‘ushindani’ wake na Wizkid unachochewa na mashabiki.

Alidai kuwa yeye na msanii huyo walikuwa marafiki wa muda mrefu ambao uhusiano wao ulidorora wakati wote waliendelea kukomaa kimwili.