Manzi wa Kibera aeleza kwa nini atamzika Nzuki na nguo zake zote na kuchora tattoo yake bandia

“Naogopa tattoo kuchora, siwezi chorwa tattoo ya mzae lakini naweza tafuta mwenye anaweza nichora ile bandia kidogo ndio nisihisi uchungu. Sijali kumchora katika sehemu yoyote kwa mwili wangu,” alisema

Muhtasari

• Kuhusu kumuenzi kwa njia nyingine ya kipekee Zaidi, Manzi wa Kibera alisema angechora tattoo ya kudumu ya mzee huyo lakini anaogopa kuhisi uchungu. 
• “Ningependa kusema ahsante mzae ulinifanya nikatrend,” Manzi wa Kibera alisema baina ya miguno ya kilio na majonzi.

Image: INSTAGRAM// MANZI WA KIBERA

Jumanne baada ya kutembelea makafani ya Nairobi na kuona mwili wa aliyekuwa mpenzi wake, Manzi wa Kibera ametoa maelezo kuhusu ni nini atafanya ili kumpa buriani ya heshima mzee huyo.

Akizungumza na waandishi wa habari nje ya makafani ya Nairobi, Manzi wa Kibera alionekana kulemezwa na hisia za majonzi na kujuta kutokuwepo karibu wakati mzee Nzuki, mwenye umri wa miaka 67 alikuwa anakata Kamba.

Mwanasosholaiti huyo alimuomboleza Nzuki akishukuru kwa nyakati ambazo walitumia pamoja kujivinjari na kusema kwamba kupitia kwake, alipata umaarufu wa kuzungumziwa mitandaoni kwenye tovuti na blogu za udaku na burudani.

“Ningependa kusema ahsante mzae ulinifanya nikatrend,” Manzi wa Kibera alisema baina ya miguno ya kilio na majonzi.

Manzi wa Kibera alifichua kwamba alikuwa akijivinjari katika ufukwe wa bahari Hindi, Pwani ya Kenya na kufichua mara ya mwisho walizungumza na Mzee Nzuki ni wakati wa Pasaka.

Alisikitika kutokuwepo karibu naye wakati alimhitaji Zaidi lakini akafichua kwamba atamzika na nguo zake zote ambazo walinunua pamoja lakini atasema atasalia na tsheti moja kama ukumbusho wake.

“Nguo zenye tulishonewa pamoja, ile tsheti nitabaki nayo niweke kwa frame lakini nguo zingine nilizovaa na yeye ndizo nitamzika nazo” Manzi wa Kibera alisema.

Kuhusu kumuenzi kwa njia nyingine ya kipekee Zaidi, Manzi wa Kibera alisema angechora tattoo ya kudumu ya mzee huyo lakini anaogopa kuhisi uchungu.

Alisema atatafakari kutafuta mtu wa kumchora tattoo bandia ambayo itafutika baada ya muda Fulani.

“Naogopa tattoo kuchora, siwezi chorwa tattoo ya mzae lakini naweza tafuta mwenye anaweza nichora ile bandia kidogo ndio nisihisi uchungu. Sijali kumchora katika sehemu yoyote kwa mwili wangu,” mwanasosholaiti huyo alieleza.

Awali, tuliripoti kuwa familia ya Mzee Nzuki ilisema inatathmini kumzika katika makaburi ya Lang’ata kutokana na kile walikitaja kuwa ni mzozo wa shamba unaotokota nyumbani kwao.