Waziri wa elimu Julius Migosi amesema kuwa mvurugano baina
ya wizara ya elimu na muungano wa wafanyakazi wa vyuo vikuu UASU kuhusiana na
fomula ya wahadhiri hao kurejea kazini
ni maelewano ya asilia 7 na 10 makundi hayo mawili yalikubaliana katika
mkataba.
Waziri Migosi akiwa mbele ya seneti kujibu maswali ya maseneta kuhusu wizara yake mnamo Jumatano amesema takwimu za fedha ambazo serikali inafahamu ikilinganishwa na fedha zinazohitajika na UASU zinatofautiana na shilingi bilioni 5.
Migosi alikuwa anajibu swali la seneta mteule Gloria Orwoba aliyetaka kufahamu ikiwa upungufu katika mgao wa fedha wizara ya elimu unahusiana na upungufu wa sasa unaosababisha kugoma kwa wahadhiri wa vyuo vikuu.
Waziri Migosi amesema kuwa taifa linakabiliwa na upungufu kwa ujumla katika bajeti ya taifa kwa kila wizara akilaumu kuangushwa kwa mswada wa fedha wa mwaka 2024/2025 kuwa chanzo cha changamoto zinazoshuhudiwa.
Akizungumzia swala la mgomo wa wahadhiri, waziri huyo amesema kuwa wizara itafanya mkutano na UASU Jumatano mchana kujadili namna ya kutatua makubaliano ya ongezeko la asilimia 7 na 10 baada ya kukosa fedha hizo.
Kulingana na Migosi, mkutano wa Jumatano unalenga kuwepo kwa makubaliano baina ya wizara na UASU kukubaliana kiwango kingine cha fedha kitakachowakilisha asilimia saba na kumi kwa kulinganisha na idadiya miaka mkataba huo utadumu.
Mkutano baina ya wizara ya elimu na UASU unajiri siku moja baada ya wahadhari ambao ni wanachama wa UASU kurejelea tena mgomo mwezi mmoja baada ya kuusitisha.
Muungano wa UASU umerejelea mgomo siku ya Jumanne baada ya kulalamikia serikali kukosa kutimiza ahadi ya maelewano ya kurejea kazini ya tarehe 26 Septemba.