
Seneta wa Kisii, Richard Onyonka, amedai kuwa kuundwa kwa serikali ya muungano mpana kumeharibu ushawishi wa kisiasa wa Raila Odinga.
Akizungumza katika mahojiano ya moja kwa moja na kituo cha runinga cha humu nchini siku ya Jumatano, Julai 16, 2025, Onyonka alisema kuwa kila mtu alikubaliana na hatua ya Raila kujiunga na serikali ya Rais William Ruto ili kusaidia kutokana na hali ya kutoeleweka serikalini.
Hata hivyo, alisema kwamba kile kilichotokea baadaye kiliwavunja moyo wengi, akifichua kuwa kama chama walifanya mashauriano na kuwasilisha mapendekezo kadhaa ya kujumuishwa katika serikali hiyo, lakini hadi sasa hakuna hata moja lililotekelezwa.
"Awali, wakati Raila alikaa nasi na kujadili kuhusu kujiunga na serikali kusaidia Rais William Ruto kwa sababu serikali haikuwa imara na kulikuwa na hali ya kutoeleweka kuhusu nini kifanyike, wengi wetu tulikuwa na mtazamo chanya," Onyonka alisema.
"Lakini kile kilichobadilika njiani kiliwakera watu wengi kwa sababu tulisema kulikuwa na mambo rahisi ambayo serikali hii na kiongozi wetu wa chama wangeweza kumwambia William Ruto, ‘tunataka kukuunga mkono lakini ita watu wako na urejeshe mambo fulani muhimu kwa Wakenya,’" aliongeza.
"Jambo lingine tulilomwambia Raila ni kwamba tunataka kuifanya nchi yetu kuwa ya haki, hatutaki kuona chaguzi zikifeli kila mara, na kwamba Ruto na Raila walipaswa kuanzisha mfumo bora wa uchaguzi.
Lakini hakuna hata jambo moja kati ya yale tuliyojadili lililowekwa katika utekelezaji. Tulikuwa tukizungumzia kuhusu utawala bora na ushirikishwaji."
Onyonka aliongeza kusema kuwa mradi wa kushirikiana na serikali ya kitaifa chini ya uongozi wa Ruto ulikuwa na nia ya kunufaisha eneo la Nyanza ambalo kihistoria limekuwa likitengwa.
Hata hivyo, alisema kuwa kwa kumwonesha Raila kama kiongozi wa jamii ya Waluo, hatua hiyo ilimharibu kisiasa na kuondoa uaminifu aliokuwa nao awali.
"Ninasema haya kwa unyenyekevu kwa kiongozi wetu wa chama Raila Odinga, ukweli ni kwamba mradi wa kushirikiana na serikali ya kitaifa ya William Ruto ulikuwa na nia mahsusi ya kulenga eneo la Nyanza, ambalo kihistoria limetengwa, na kwa kumtambua kama kiongozi wa Waluo, ilimharibu na kuondoa uaminifu aliokuwa ameujenga," aliongeza.