logo

NOW ON AIR

Listen in Live

Kalombotole Akamatwa na Polisi Kufuatia Mauaji ya Mgonjwa Katika Hospitali ya Kenyatta

Polisi wamemkamata mwanaume mmoja kuhusiana na kifo cha mgonjwa aliyeaga dunia katika mazingira yasiyoeleweka.

image
na Tony Mballa

Habari18 July 2025 - 09:02

Muhtasari


  • Uchunguzi wa awali unaonyesha kuwa Kennedy Kalombotole alilazwa hospitalini hapo mnamo Desemba 1, 2024, na ndiye mshukiwa mkuu katika mauaji ya Gilbert Kinyua Muthoni, mwenye umri wa miaka 40, aliyeuawa katika Wodi ya 7C usiku wa Februari 6 hadi 7, 2025.
  • Baada ya tukio hilo, jalada la uchunguzi liliwasilishwa kwa Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (ODPP). Hata hivyo, baada ya kulikagua, ODPP ilielekeza afisa anayechunguza kesi hiyo kufanya uchunguzi wa ziada ili kuimarisha kesi hiyo ya mashtaka.

Polisi wamemkamata mwanaume mmoja kuhusiana na kifo cha mgonjwa aliyeaga dunia katika mazingira yasiyoeleweka katika Hospitali ya Kitaifa ya Kenyatta (KNH).

Maafisa wa upelelezi wa mauaji wamemtambua mshukiwa huyo kama Kennedy Kalombotole, wakieleza kuwa ndiye mshukiwa mkuu katika mauaji ya kikatili yaliyotokea kwenye wodi ya hospitali hiyo.

Anahusishwa na mauaji ya Edward Maingi Ndegwa mnamo Julai 17, 2025.

“Kulingana na taarifa za awali, muuguzi wa wodi alimkagua mgonjwa saa 5:30 asubuhi na kupima shinikizo lake la damu. Saa 6:30 mchana, jamaa wa mgonjwa alimtembelea na kumkuta akiwa katika hali nzuri na akaondoka wodi hiyo saa 7:30. Hata hivyo, takriban saa 8:00 mchana, mfanyakazi wa usafi aliyekuwa akifagia korido aliona damu ikitoka kwenye shingo ya mgonjwa huyo,” taarifa kutoka DCI ilisoma.

“Wachunguzi walipofika katika eneo la tukio waliona alama za raba zenye damu kuanzia pembeni mwa kitanda cha marehemu hadi choo kilicho karibu, kisha hadi kwenye chumba cha pembeni ambacho mshukiwa, Kalombotole, alikuwa amelazwa. Katika chumba hicho, wachunguzi walipata jozi ya raba za buluu na shuka lililokuwa na doa la damu.”

“Pia, sakafuni moja kwa moja kuelekea ghorofa ya saba ambapo dirisha la wodi aliyolazwa marehemu lilipo, walipata kisu kilichokuwa kimefungwa kwa glovu.”

Vitu vilivyopatikana vilipelekwa katika Maabara ya Kitaifa ya Uchunguzi wa Kisayansi kwa uchunguzi wa kina ili kuimarisha ushahidi wa kesi hiyo.

Kennedy Kalombotole

Uchunguzi wa awali unaonyesha kuwa Kennedy Kalombotole alilazwa hospitalini hapo mnamo Desemba 1, 2024, na ndiye mshukiwa mkuu katika mauaji ya Gilbert Kinyua Muthoni, mwenye umri wa miaka 40, aliyeuawa katika Wodi ya 7C usiku wa Februari 6 hadi 7, 2025.

Baada ya tukio hilo, jalada la uchunguzi liliwasilishwa kwa Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (ODPP). Hata hivyo, baada ya kulikagua, ODPP ilielekeza afisa anayechunguza kesi hiyo kufanya uchunguzi wa ziada ili kuimarisha kesi hiyo ya mashtaka.

Kalombotole kwa sasa yuko kizuizini na uchakataji wa kesi yake unaendelea kabla ya kufikishwa mahakamani.

Katika taarifa ya hospitali ya Kenyatta iliyotolewa Alhamisi, Julai 17, 2025, ilielezwa kuwa mgonjwa alipatikana katika wodi ya matibabu akiwa amelala kwenye mashuka yaliyokuwa yamejaa damu na alithibitishwa kuwa amefariki baada ya uchunguzi kufanyika.

“Tunasikitika sana kuthibitisha tukio la kifo cha kusikitisha cha mgonjwa katika Hospitali ya Kitaifa ya Kenyatta. Alasiri ya Julai 17, 2025, takriban saa 8 mchana, mara baada ya muda wa kuwatembelea wagonjwa kumalizika, mgonjwa alipatikana katika wodi ya matibabu akiwa amelala juu ya mashuka yaliyolowa damu. Mgonjwa alikaguliwa na kuthibitishwa kuwa amefariki dunia,” sehemu ya taarifa hiyo ilisoma.

Hospitali ilithibitisha pia kuwa suala hilo liliripotiwa kwa Idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI) pamoja na mashirika mengine ya usalama ya serikali.

“Tukio hilo limeripotiwa kwa Idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI) na mashirika mengine husika ya usalama ya serikali,” taarifa hiyo iliongeza.

“Mawazo na sala zetu ziko na familia ya marehemu katika kipindi hiki kigumu. Tutatoa taarifa zaidi kadri tutakavyopokea.”

Hospitali haijataja jina la marehemu wala hali yake ya kiafya, ikitaja sababu za faragha na uchunguzi unaoendelea.

Gilbert Kinyua

Tukio hili linajiri miezi michache baada ya DCI kutangaza kuwa wachunguzi kutoka kitengo cha mauaji walikuwa wakichunguza mauaji ya mgonjwa ndani ya wodi katika hospitali hiyo.

Gilbert Kinyua, mwenye umri wa miaka 39, aliuawa kikatili ndani ya Wodi ya 7B mnamo Februari 7, 2025, na mshambuliaji ambaye bado hajafahamika.

Mwili wake usio na uhai ulipatikana kitandani, shingo ikiwa imechanwa kwa kisu, asubuhi ya Ijumaa, Februari 7, 2025.

Kinyua alikuwa amelazwa KNH mnamo Desemba 11, 2024, kutokana na tatizo la kiafya la ubongo. Takriban mwezi mmoja baadaye, mwili wake ulikutwa katika dimbwi la damu ndani ya wodi ya hospitali — tukio lisilotarajiwa katika mazingira ya hospitali.

Katika wodi aliyokuwa amelazwa Gilbert, mgonjwa mwingine alikuwa pia akitibiwa kwa hali hiyo hiyo. Hata hivyo, mgonjwa huyo alikuwa dhaifu na hakuweza kueleza chochote kuhusu yaliyotokea kabla na baada ya tukio hilo la kushangaza.

Muuguzi aliyekuwa kazini usiku huo alieleza kwa wachunguzi kuwa alifanya ukaguzi wa kawaida saa 9 usiku na kila kitu kilikuwa sawa.

Saa 12 asubuhi siku hiyo hiyo, aliporejea katika wodi alimkuta Gilbert akiwa amefariki kitandani, shingo ikiwa imechanwa na damu ikimwagika kila mahali.

Maafisa wa Kitengo cha Upelelezi wa Mauaji waliarifiwa.

Walipowasili, walipata kisu cha jikoni chenye damu ambacho kilitupwa hadi ghorofa ya chini kupitia dirisha lililokuwa karibu na sehemu ambapo Gilbert aliuawa.

Wapelelezi walikuwa eneo la tukio wakijaribu kuunda upya mlolongo wa matukio huku wakikusanya picha za CCTV kutoka maeneo ya jirani.

Makala Zinazohusiana


RADIO JAMBO FREQUENCIES

Kisumu 100.1 | Mombasa 92.3 | Nakuru 96.9 | Eldoret 99.5 | Nyeri 99.3 | Nyahururu 97.3 | Webuye 95.3 | Meru 92.7 | Kitui 104.9 | Kibwezi 104.7 | Voi 105.7 | Malindi 98.1 | Lamu 104.7 | Narok 97.3 | Kapenguria 99.7 | Kisii 89.3 | Garissa 104.3 | Maralal 97.3 | Lodwar 92.7


logo© Radio Jambo 2024. All rights reserved