logo

NOW ON AIR

Listen in Live

Ruto: Msikubali Kuongozwa na Watu Wasio na Mpango

Rais alisema kuwachochea vijana kufanya vurugu na kuharibu mali si njia mbadala ya kuunda ajira.

image
na Tony Mballa

Habari18 July 2025 - 07:21

Muhtasari


  • Mpango wa Climate WorX umeunda ajira 200,000 kote nchini, huku zaidi ya 320,000 wakifanya kazi katika mpango wa Makazi Nafuu. Idadi hii, alisema, itaongezeka mara mbili ndani ya miezi mitatu ijayo.
  • Aliongeza kuwa tayari watu 400,000 wamepata ajira kupitia mpango wa uhamaji wa kazi, huku 180,000 wakiwa kwenye ajira za kidijitali, miongoni mwa nyinginezo.

Rais William Ruto amewataka wapinzani wake kuweka wazi mipango yao mbadala ya uundaji wa ajira kwa vijana.

Akizungumza katika eneo la Dandora alipokuwa akikagua mradi wa kufufua Mto Nairobi, Rais Ruto aliwahimiza vijana kuwakataa viongozi wasio na ajenda ya taifa wala suluhu kwa changamoto kama ukosefu wa ajira.

"Msikubali kuongozwa na viongozi wasio na mpango wowote, na ambao wanasukumwa na ukabila na chuki," alisema Rais Ruto.

Rais alisema kuwachochea vijana kufanya vurugu na kuharibu mali si njia mbadala ya kuunda ajira.

Alisema ana mpango madhubuti ambao tayari umeanza kuunda mamia ya maelfu ya nafasi za ajira kwa vijana, kinyume na wapinzani wake ambao, kwa mujibu wake, hawana mpango wowote.

Mpango wa Climate WorX umeunda ajira 200,000 kote nchini, huku zaidi ya 320,000 wakifanya kazi katika mpango wa Makazi Nafuu. Idadi hii, alisema, itaongezeka mara mbili ndani ya miezi mitatu ijayo.

Aliongeza kuwa tayari watu 400,000 wamepata ajira kupitia mpango wa uhamaji wa kazi, huku 180,000 wakiwa kwenye ajira za kidijitali, miongoni mwa nyinginezo.

"Mpango wenu ni upi? Hauwezi kuwa mpango wenu ni kuchochea na kuwalipa vijana waharibu mali na kuchoma biashara. Hiyo haikubaliki," alisisitiza.

Rais alisema amejitolea kuunganisha Wakenya wote na kutokomeza ukabila na mgawanyiko miongoni mwa wananchi.

Alifafanua kuwa mazingira yenye vurugu na machafuko hayawezi kuwezesha uundaji wa ajira wala maendeleo ya kitaifa.

"Hatuna muda wa vurugu, machafuko na ukabila. Tunataka kujenga nchi yetu," alisema.

Aliahidi kuhakikisha kuwa taifa linaungana katika ajenda ya maendeleo badala ya siasa zisizoisha ambazo wapinzani wake wanapendelea.

"Kama kiongozi wa taifa hili, nitahakikisha hakuna Mkenya anayebaguliwa, na hakuna jamii au eneo linaloachwa nyuma," alisema.

Rais aliwahimiza Wakenya kujisajili katika Mamlaka ya Bima ya Afya ya Jamii (SHA) na akaahidi kuimarisha taasisi hiyo ili iwahudumie Wakenya wote.

"Nitahakikisha SHA inafanya kazi, na kila anayekwenda hospitali anatibiwa na SHA inalipa gharama," alisema Rais Ruto.

Rais alibainisha kuwa mradi wa kufufua Mto Nairobi tayari umeunda nafasi 20,000 za ajira kwa vijana wa Kaunti ya Nairobi.

Rais William Ruto

Aliongeza kuwa vijana wengine 20,000 wataanza kazi Jumatatu ijayo, na kufanya jumla ya vijana waliopata ajira kupitia mradi huo kufikia 40,000 jijini Nairobi.

Mradi huo utajumuisha ujenzi wa kilomita 54 za miundombinu mipya ya maji taka kandokando ya Mto Nairobi ili kuzuia uchafu wa majitaka kuingia mtoni.

Pia utahusisha ujenzi wa nyumba za makazi ya kijamii 10,000 mwanzoni kando ya mto, pamoja na bustani za jamii, kumbi za kijamii na vyoo vya umma.

Mpango wa Climate WorX utajumuisha ujenzi wa njia za waenda kwa miguu na wapanda baiskeli kando ya mto, kuweka umeme katika njia hizo na bustani, na ujenzi wa madaraja 44 ya waenda kwa miguu yasiyo ya magari.

Aidha, kiwanda cha kusafisha maji taka cha Kariobangi kitapanuwa uwezo wake ili kuboresha usafishaji wa majitaka.

Masoko ya kisasa yatajenziwa wafanyabiashara, na miti itapandwa kando ya mito ili kukabiliana na mmomonyoko wa udongo na kuhifadhi mazingira.

Mbali na mpango wa makazi, ambao utatekelezwa kote jijini, miradi yote ya awamu ya kwanza itatekelezwa katika sehemu ya urefu wa kilomita 27.2 wa Mto Nairobi kutoka Naivasha Road hadi Dandora Falls.

Mito ya Mathare na Ngong itahusishwa katika awamu ya pili ya mpango huo.

Rais Ruto alieleza kuwa mradi wa kufufua Mto Nairobi pia utahusisha uvuvi wa maji baridi, mifumo ya majitaka, masoko, na nyumba za kijamii, na yote yanatarajiwa kukamilika kufikia tarehe 15 Januari, 2027.

Awali, Rais alizindua barabara ya daraja la Savannah Stage 17, linalopita kati ya maeneo bunge ya Embakasi Central na Embakasi East.

Alisema kuwa serikali inatekeleza mpango kamili wa kuibadilisha Nairobi kuwa kituo cha kimataifa cha hali ya juu.

Katika awamu ya kwanza, serikali inajenga angalau kilomita 70 za barabara jijini ili kurahisisha biashara, kupunguza msongamano wa magari, na kuharakisha ukuaji.

Gavana wa Nairobi Johnson Sakaja alisema wakaazi wamekataa siasa za ukabila na sasa wanaungana kubadilisha jiji hilo.

Viongozi wengine waliokuwepo ni Naibu Gavana wa Nairobi James Muchiri, wabunge Phelix Odiwuor (Lang’ata), TJ Kajwang (Ruaraka), George Aladwa (Makadara), Anthony Olouch (Mathare), pamoja na wabunge walioteuliwa Karen Nyamu na Maureen Mutinda.

Makala Zinazohusiana


RADIO JAMBO FREQUENCIES

Kisumu 100.1 | Mombasa 92.3 | Nakuru 96.9 | Eldoret 99.5 | Nyeri 99.3 | Nyahururu 97.3 | Webuye 95.3 | Meru 92.7 | Kitui 104.9 | Kibwezi 104.7 | Voi 105.7 | Malindi 98.1 | Lamu 104.7 | Narok 97.3 | Kapenguria 99.7 | Kisii 89.3 | Garissa 104.3 | Maralal 97.3 | Lodwar 92.7


logo© Radio Jambo 2024. All rights reserved