Kimbunga Hidaya kuendelea kusogea ukanda wa Pwani ya Tanzania leo

TMA imesema kimbunga Hidaya kitaendelea kusogea karibu kabisa na ukanda wa pwani wa Tanzania mchana wa Jumamosi.

Muhtasari

•Mamlaka imesema mpaka kufika saa tatu ya siku ya jana, kimbunga kilikuwa katika eneo la bahari takribani kilomita 230 kutoka pwani ya Kilwa.

Image: BBC

Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imetoa taarifa ya mwenendo wa kimbunga Hidaya kilichopo katika Bahari ya Hindi mashariki mwa pwani ya Tanzania.

Mamlaka imesema mpaka kufika saa tatu ya siku ya jana, kimbunga kilikuwa katika eneo la bahari takribani kilomita 230 kutoka pwani ya Kilwa (Mkoa wa Lindi) na kilomita 170 kutoka pwani ya Mafia kikiwa na kasi ya upepo inayofikia kilomita 120 kwa saa.

Uwepo wa kimbunga karibu na pwani ya nchi hiyo umeendelea kutawala mifumo ya hali ya hewa katika baadhi ya maeneo ambapo katika kipindi cha saa 12 zilizopita, vipindi vya mvua kubwa na upepo mkali vimeendelea kujitokeza.

Hali ya upepo mkali unaozidi kilomita 40 kwa saa imeelezwa kujitokeza katika vituo vya hali ya hewa Mtwara, Kilwa, Zanzibar na Dar es Salaam na mvua kubwa Lindi na Mtwara.

TMA imesema kimbunga Hidaya kitaendelea kusogea karibu kabisa na ukanda wa pwani wa Tanzania mchana wa leo tarehe 4 Mei kabla ya kuanza kupungua nguvu kuelekea siku ya kesho.

Kwa siku ya leo, kimbunga kinatarajiwa kuendelea kusababisha matukio ya vipindi vya mvua kubwa na upepo mkali katika maeneo ya ukanda wa pwani hususani mikoa ya Lindi, Mtwara, Pwani na Dar es Salaam pamoja na visiwa vya Unguja na maeneo jirani.