Kenya Power itaadhibiwa ikiwa kukatika kwa umeme kutazidi mara 20 kwa mwaka

Kama njia moja ya kupunguza kiasi cha muda ambao umeme hupotea, EPRA inapendekeza muda wa kupotea kwa umeme bila kutarajiwa ukienda sana uwe ni kwa saa 80 tu ndani ya mwaka mzima.

Muhtasari

• Hata hivyo, itakumbukwa kwamba masharti hayo mapya hayatakuwa yakifanya kazi kwa kukatishwa kwa umeme kulikoratibiwa.

• KPLC aghalabu hutangaza kukatika kwa umeme ili kupisha njia kwa marekebisho ya mitambo yao ya usambazaji umeme.

Mtambo wa nyaya za stima
Mtambo wa nyaya za stima
Image: Screenshot

Kmapuni ya kitaifa ya kusambaza umeme, KPLC itajipata pabaya na kukabidhiwa adhabu kali ikiwa kukatika kwa umeme kutazidi mara 20 ndani ya mwaka mmoja, EPRA imetangaza.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo iliyochapishwa kwenye toleo la Nation, EPRA inapendekeza kuwekwa kwa kikomo cha ni mara ngapi mifumo ya umeme nchini itapata hitilafu za kupelekea kupotea kwa umeme, hadi mara 20 pekee ndani ya mwaka mmoja.

Kwa mujibu wa EPRA, pendekezo hili linanuia kuboreshwa kwa huduma za KPLC kwa watumizi wake.

Pendekezo hili jipya litaweka shinikizo kwa KPLC kuboresha mitambo yao na mifumo ya kusambaza umeme ili kuzuia kukatika ovyo kwa umeme mara kwa mara, jambo ambalo linatajwa kuvuruga biashara nyingi zinazotegemea nguvu za umeme haswa nyakati za usiku na viwandani nyakati za mchana.

Kama njia moja ya kupunguza kiasi cha muda ambao umeme hupotea, EPRA inapendekeza muda wa kupotea kwa umeme bila kutarajiwa ukienda sana uwe ni kwa saa 80 tu ndani ya mwaka mzima.

Nation walibaini kwamba ikiwa pendekezo hili litaanza kufanya kazi, hili litakuwa ni boresho kubwa ikizingatiwa kwamba kwa sasa umeme hupotea nchini kwa takribani saa 115.73 ndani ya mwaka mzima.

Pia pendekezo hilo limeweka kikomo cha kupotea kwa umeme kila mara kutozidi saa 4, ambapo itakuwa ni boresho kutoka kwa muda wa sasa wa kupotea kwa umeme unaokwenda hadi saa 4 na dakika 52.

Hata hivyo, itakumbukwa kwamba masharti hayo mapya hayatakuwa yakifanya kazi kwa kukatishwa kwa umeme kulikoratibiwa.

KPLC aghalabu hutangaza kukatika kwa umeme ili kupisha njia kwa marekebisho ya mitambo yao ya usambazaji umeme.