Wanaume 5 wakatwa vichwa na washambuliaji wa al Shabaab katika vijiji vya Lamu

Wanawake waliongozwa hadi vyumba tofauti na baadaye kuachiliwa huru.

Muhtasari

•Mwanafunzi aliyeuawa alikuwa amekuja nyumbani kwa mapumziko ya nusu muhula kabla ya kukutana na kifo chake.

• Kundi la wanaume zaidi ya 30, waliokuwa na bunduki, mapanga na visu walishambulia mapema jioni.

Image: BBC

Takriban wanaume watano walikatwa vichwa na nyumba nyingi kuteketezwa katika shambulio la al Shabaab katika vijiji vya Salama na Juhudi katika eneo la Mkunumbi, Kaunti ya Lamu.

Mashahidi na polisi walisema wavamizi hao walivamia vijiji hivyo mwendo wa saa moja unusu usiku wa Jumamosi, na kuwatoa waathiriwa kutoka kwenye nyumba zao na kuwafunga mikono na miguu kwa kamba nyuma ya migongo yao kabla ya kuwaua.

Wahasiriwa wa shambulio hilo la Jumamosi usiku wote ni wanaume, akiwemo mwanafunzi wa Kidato cha Tatu kutoka Shule ya Sekondari ya Bakania aliyetambulika kama Barack Hussein, 19.

Mwanafunzi huyo alikuwa amekuja nyumbani kwa mapumziko ya nusu muhula kabla ya kukutana na kifo chake.

Vikosi vya usalama vya kaunti ya Lamu vilifika eneo la tukio muda mfupi baadaye lakini hakuna aliyekamatwa.

Kamishna wa Kaunti, Louis Rono alisema anafahamu kuhusu shambulio hilo katika kijiji cha Salama lakini hakuwa na maelezo zaidi.

"Ndio kulikuwa na shambulio katika kijiji na tunaelekea huko," alisema bila kutoa maelezo zaidi.

Mashahidi na polisi walisema kundi la wanaume zaidi ya 30, waliokuwa na bunduki, mapanga na visu walishambulia mapema jioni.

Mashahidi walisema watu hao walikuwa wamevalia mavazi ya kijeshi walipovamia nyumba hizo. Kisha wakaamuru waliokuwepo walale chini na wasiitane..

Wanawake waliongozwa hadi vyumba tofauti na baadaye kuachiliwa huru. Wavamizi hao waliwachinja watano hao na baadaye kuiba baadhi ya vyakula, kuku na mbuzi kabla ya kuchoma moto duka.

Eneo hilo limekuwa miongoni mwa maeneo yenye wasiwasi kwa sababu ya hofu ya mashambulizi kutoka kwa kundi la kigaidi.