Wakili Ahmednasir ajigamba uwepo wake Emirates ulisaidia Arsenal kupiga Chelsea 5-0

Ahmednasir alitazama moja kwa moja wakati Wanabunduki wakiwachapa The Blues 5-0 uwanjani Emirates.

Muhtasari

•Wakili Ahmednasir alikuwa katika uwanja wa Emirates siku ya Jumanne usiku wakati Arsenal ilipowashinda majirani zao Chelsea 5-0 .

•Mchezo ulipokuwa ukiendelea, mwanasheria huyo mashuhuri alionyesha video na picha za matukio makubwa ya mechi hiyo.

Image: TWITTER// AHMEDNASIR ABDULAHHI

Wakili mashuhuri wa Kenya Ahmednasir Abdullahi alikuwa katika uwanja wa Emirates siku ya Jumanne usiku wakati klabu yake anayoipenda zaidi Arsenal ilipowashinda majirani zao Chelsea 5-0 katika mechi ya kusisimua iliyochezwa mwendo wa saa nne.

Wakili huyo alitumia akaunti yake ya Twitter yenye wafuasi zaidi ya milioni 2.3 kuwafahamisha mashabiki wake kuhusu ziara yake katika uwanja huo maridadi wa London, nchini Uingereza.

Alichapisha picha zake akiwa amesimama kwenye eneo la kuketi wakati wa mechi hiyo na akajigamba kwamba uwepo wake katika uwanja wa Emirates ulisaidia klabu yake anayoipenda zaidi kuwapa wapinzani wao kichapo cha mbwa.

"Nina furaha kwamba uwepo wangu kwenye Uwanja wa Emirates uliinua ari ya timu... nilitaka mabao ya tarakimu mbili, lakini 5.0 ni sawa," Ahmednasir alisema.

Mchezo ulipokuwa ukiendelea, mwanasheria huyo mashuhuri alionyesha video na picha za matukio makubwa ya mechi hiyo.

Siku ya Jumanne usiku, Chelsea ilipata kichapo kikubwa na chungu kutoka kwa wapinzani wao wakubwa Arsenal katika mechi ya kusisimua iliyochezwa kwenye Uwanja wa Emirates jijini London, Uingereza.

Vijana wa Mauricio Pochettino walishindwa kufunga bao lolote huku wapinzani wao wa usiku wa Jumanne wakifunga mabao matano dhidi ya kipa Djordje Petrovic.

Mchezaji wa Kimataifa wa Ubelgiji Leandro Trossard alifunga bao la kwanza la  Wanabunduki dakika nne tu baada ya mchuano kuanza.

Timu zote zilipata nafasi kadhaa za kufunga katika dakika zilizosalia za kipindi cha kwanza lakini hakuna hata mmoja wao aliyebadilisha nafasi hizo kuwa mabao.

Ilikuwa ni kipindi cha pili ambapo Wanabunduki walionyesha ukali wa risasi zao huku wakifunga mabao manne zaidi na kuwashinda majirani zao jijini London.

Mshambulizi wa zamani wa Chelsea, Kai Harvetz na beki wa kulia wa Uingereza, Ben White walifunga mabao mawili kila mmoja na kuipa Arsenal ushindi muhimu wakati wanapigania kombe la EPL 2023/34 na Manchester City na Liverpool.

Ushindi wa Jumanne jioni uliwapeleka vijana wa Mikel Arteta kileleni mwa jedwali wakiwa na pointi 77 na pia kuboresha tofauti yao ya mabao.

Manchester City hata hivyo wana michuano miwili ambayo hawajacheza ambayo inaweza kuwapeleka kileleni mwa jedwali iwapo watashinda.

 Kwa upande wao, Liverpool wana mchuano mmoja ambao haujachezwa na ushindi utawafanya wao na Arsenal kuwa sawa kwa pointi.