Familia ya Dani Alves yavunja kimya kufuatia uvumi kwamba amejitoa uhai gerezani

Uvumi kwamba Alves alijitoa uhai ndani ya jela ambako amefungwa uliibuka siku ya Jumamosi jioni

Muhtasari

•Familia ya mchezaji Dani Alves imezika tetesi zinazodai kuwa mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 40 amefariki.

•Bw Nay Alves alichapisha jumbe na picha zaidi kuhusu hali ya kakake gerezani na kuwatuliza mashabiki .

amefungwa jela miaka minne unusu
Beki Dani Alves amefungwa jela miaka minne unusu
Image: HISANI

Familia ya staa wa zamani wa Barcelona na Brazil Dani Alves imezika tetesi zinazodai kuwa mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 40 amefariki.

Uvumi kwamba Alves alijitoa uhai ndani ya jela ambako amefungwa kwa miaka minne unusu baada ya kupatikana na hatia ya ubakaji uliibuka siku ya Jumamosi jioni baada ya mwanamtandao kuchapisha kuhusu hilo.

Siku ya Jumapili, Nay Alves, kaka wa mwanasoka huyo wa zamani wa Brazil hata hivyo alitoa taarifa akiuhakikishia ulimwengu kuwa mwanasoka huyo yu hai na hajajitoa uhai kama ilivyodaiwa. Pia alichukua fursa hiyo kuwakashifu walioibua madai hayo ya kuhuzunisha

"Binadamu ni wakatili kiasi gani. Tayari alihukumiwa kwa maneno ya mwanamke aliyeingia kwenye chumba cha wanaume kufanya kile anachojua yeye tu na yeye. Tayari ameshahukumiwa, haitoshi?" kaka wa mchezaji huyo wa zamani aliandika kwenye Instagram akisindikizwa na picha ya wawili hao wakiwa pamoja.

Aliongeza, "Haitoshi. Sasa kichaa wanataka kumuona amekufa, vipi wewe ukatili sana? Baba yangu ana zaidi ya miaka 70. Mama yangu ana zaidi ya miaka 60. Hawana familia, je! Kurasa hizi zinaendelea kueneza mambo haya."

Bw Nay Alves alichapisha jumbe na picha zaidi kuhusu hali ya kakake gerezani na kuwatuliza mashabiki waliokuwa wameamini habari za kufariki kwake

Mahakama moja nchini Uhispania ilimpata Dani Alves na hatia ya kumbaka mwanamke katika klabu ya usiku ya Barcelona. Baadaye alihukumiwa kifungo cha miezi minne na sita jela mnamo Februari 22, na hata zaidi alihukumiwa miaka mitano ya uhuru unaosimamiwa, na kusitisha mawasiliano yote na mwathiriwa kwa miaka tisa na miezi sita.

Aidha, alitakiwa lazima alipe fidia ya euro 150,000 na gharama za kesi. Mwanasoka huyo wa zamani tayari ametumikia kifungo cha mwaka mmoja, mwezi mmoja na siku 18 jela.