Jane Nambuye Manyonge alihukumuiwa kifo Mei tarehe 30 mwaka wa 2017 na jaji Stella Mutuku baada ya kupatikana na hatia ya kumuua mume wake Francis Mulumeti nyumbani kwao Riruta Dagoretti mwaka wa 2013.
Mulumeti alikuwa akifanya kazi katika wizara ya ugatuzi ilhali Manyonge alikuwa mwalimu katika shule ya Le Pic School mtaani Dagoretti.
Ikipunguza hukumu yake, mahakama ya rufaa imesema sio lazima korti itoe adhabu ya juu zaidi ya kifo kama ilivyoratibiwa katika sheria.
Mfano huo mpya unafaa kutumiwa kwa kesi baada ya kesi wala haufai kutumiwa kwa kesi zote za mauaji. Wakati wote wa kesi yake, mwalimu huyo mwenye umri wa miaka 51 alikana kumuua mume wake lakini jaji amesema ushahidi uliowasilishwa kortini ulimtwika kosa hilo .
Hii ni kwa sababu mshukiwa na mwathiriwa ndio waliokuwa watu pekee katika nyumba yao wakati wa tukio hilo kabla ya mwanamme huyo kupatikana ameaga dunia. Pia kulikuwa na damu katika nyumba yote na kuna kisu kilichopatikana na damu katika nyumba yao. Jane pia alitoa taarifa zinazokinzana kuhusu hali iliyopelekea kifo cha mumewe kwani mwanzoni mlinzi wao wa lango alikuwa amesema kwamba mwanamme huyo alianguka kwenye stuli na kufa lakini baadaye Jane akasema mume wake alikuwa amelalamikia maumivu ya kifua. Baadaye alikiri kwamba walikuwa na ndoa yenye ugomvi .
