Polisi katika kaunti ya Bungoma wameanzisha msako wa majangili 10 ambao walitoroka kutoka kituo Kikuu cha Polisi cha Bungoma.
Polisi wanasema kundi hilo lilitoroka mwendo wa saa tisa asubuhi hii leo baada ya kuchimba shimo ukutani wakati wa usiku.
Maafisa wa usalama walifanikiwa kumkamata mtuhumiwa mmoja ambaye alipigwa risasi kwenye paja alipokuwa akijaribu kutoroka.
Hayo yakijiri wizara ya masuala ya ndani hapo kesho itazindua kampeni ya usafishaji wa vituo vyote vya polisi na magereza, huku zoezi hilo likianzishwa katika kaunti ya Nairobi. Waziri Fred Matiang'i anasema hii ni sehemu ya mradi wa serikali unaoendelea unaonuwia kuboresha utoaji huduma kwa wakenya.
Kwingineko, wakaazi wa jiji la Nairobi kuanzia kesho wataweza kupata huduma za serikali katika kituo cha Huduma Center cha GPO baada ya kituo hicho kufungwa yapata mwezi mmoja sasa ii kufukizwa dawa kutokana na ongezeko la visa vya Corona jijini. Hata hivyo ili kupunguza msongamano na muda unautumia ukipanga foleni, utahitajika kupanga miadi kwanza. Ili kupanga miadi, tembelea tovuti www.hudumakenya.go.ke, bonyeza weka miadi au book appointment kisha fuata hatua za jinsi ya kuweka miadi ya huduma inayotaka.
