Wivu wa kimapenzi ni kitu kizuri lakini ukizidisha kipimo basi ni smu katika uhusiano au ndoa
Ndio masaibu ambayo amejikuta ndani Joan Njagi kwani alichofikiri ni kupendwa Zaidi sasa kimegeuka kuwa donda sugu katika ndoa yake na mumke wake Willy . Anasema mwanzoni mwa ndoa yao hakuwa na tatizo mume wake kumuuliza maswali mengi kuhusu kila alichokuwa akifanya au ameenda wapi au ametoka wapi . Wakati huo alijiambia labda kwa sababu ya kutaka kuwa karibu naye ,mume wake alikuwa na hofu ndogo ndogo za kutaka kujua mke wake yuko wapi na nani .
Lakini mambo yamegeuka na mtindo huo umeendelea hadi sasa ambapo imekuwa ni tatizo kwa rafiki na jamaa zake . Joan anasema kuna rafiki zake na hata wenzake kazini ambao wanaogopa kutangamana naye kwa sababu wanahofia kupigiwa simu na mume wake akiwauliza kuhusu wanachosema na Joan katika simu . Wakati mwingine mambo yalikuwa mabaya hadi wakati anapotoka kazini ,anampata mume wake kwenye lango kuu la afisi yao akimngoja huku akinyemelea kuona Joan atatoka na nani . Ilianza kuwa zile filamu za kuogofya ambapo mtu anaanza kukufuata gizani ma nyakati nyingi Joan alianza kuhisi kana kwamba kuna mtu anamchunguza ama kufuatilia kila alichokuwa akifanya .
Kilichovunja uvimilivu wake hata hivyo ni wakati mume wake alipomfuata siku moja hadi kwenye duka kuu ili kujua anazungumza vipi na watu . Baadaye alianza kumuambia Joan kwamba anafaa kuthibiti tabasamu yake kwa sababu alikuwa mwepesi wa ‘kumchekea kila mwanamume’. Joan alishangaa kwani alishindwa alitoa wapi dhana hiyo kumbe jamaa alikuwa amemfuata hadi katika duka kuu na kuona jinsi Joan alivyokuwa akitangamana na wahudumu pale akiwauliza vitu Fulani viko wapi na kawaida yake Joan ni mtu mwenye furaha na anajua kusema na watu lakini kwa mume wake hiyo ni hatia kwa sababu tabia hiyo ‘inawakaribisha’ wanaume kuanza kumtongoza .
Juhudi zake kujaribu kulipeleka suala hilo kwa mhubiri wa kanisa wao ili mume wake aweze kupata usaidizi wa ushauri hazijafua dafu na pindi anapofika nyumbani ,mume wake amejitayarisha kwa msururu wa maswali kuhusu njia aliopitia akitoka kazini na mtu aliyezungumza naye . Imekuwa kazi kubwa sasa kuanza kujibu maswali hayo na kupigiwa simu kila mara akiulizwa anafanya nini , na nani wapi. Kunao watu ambao wana tabia hizo na wakati mwingi uhusiano kama huo huwa hadumu na matatizo yanajaa chungu nzima .