Ann Kananu siku ya Jumatatu alichukuwa usukani kuongoza kaunti ya Nairobi kama kaimu Gavana wa kaunti hiyo siku tatu tu baada ya kuapishwa kuwa naibu gavana.
Spika wa Bunge la Kaunti ya Nairobi Benson Mutura Jumatatu alimkabidhi Kananu rasmi zana za mamlaka katika hafla iliyoandaliwa katika makau makuu ya jiji la Nairobi City Hall.
Mutura alisema kwa sababu Nairobi sasa ina Naibu Gavana hana budi kuachilia mamlaka kama Kaimu Gavana na kurejelea majukumu yake kamili kama Spika.
"Mimi sio mwanasiasa, na sitaanza kuwa mmoja. Ninalenga kuleta azma mpya ya ushirikiano, ushirikiano na kuheshimiana na idara zote za serikali. Nairobi sasa imerejea kwa mkondo wa maendeleo," Kananu alisema.
Kananu ataendelea kushikilia nafasi yake kama naibu gavana akisubiri uthibitisho kama Gavana wakati kamati ya ukabidhi wa mamlaka itakapokamilisha mchakato wa ubadilishanaji mamlaka.
Ijumaa iliyopita, Kamati ya Uteuzi iliyoongozwa na Kiongozi wa Wengi Abdi Guyo ilimpiga msasa na kumuidhinisha Kananu kuhudumu kama naibu gavana.
Katika hotuba yake ya kwanza kama naibu gavana, Kananu alisema atafanya kazi bila kuchoka pamoja na mkurugenzi mkuu wa Huduma ya Metropolitan ya Nairobi Meja Jenerali Mohammed Badi kuhakikisha kazi zote zilizohamishwa zinaimarishwa zaidi kuhakikisha huduma zinatolewa kwa wakaazi wa Nairobi.
Kananu pia aliahidi kuunda kamati ya uhusiano kati ya kaunti na NMS ili kuimarisha tendakazi wa jiji la Nairobi.