Mtangazaji Joyce Omondi amekuwa wa hivi punde kuajiriwa na runinga ya Citizen ili kuziba nafasi ya mtangazaji Kambua aliyeondoka runingani humo baada ya kuwa mtangazaji wa kipindi cha injili, Rauka kwa zaidi ya mwongo mmoja.
Omondi ambaye ni mkewe mwanahabari Wahiga Mwaura ambaye pia anafanya kazi katika runinga hiyo ya Citizen kama mhariri mkuu, amepata kazi katika kituo hicho baada ya kuondoka kwenye kituo cha runinga cha Switch mwishoni mwa mwaka 2020, Kituo ambacho kilikuja kufungwa mwaka mmoja baadaye mwishoni mwa mwaka 2021.
Omondi hatakuwa mgeni katika runinga ya Citizen kwani aliwahi fanya kazi huko na aliondoka miaka minane iliyopita kwa kile alichokitaja kuwa ni kujiendeleza kimasomo nchini Marekani.
Katika tangazo lililopeperushwa kwenye runinga ya Citizen, Omondi anatarajiwa kurejelea kuongoza kipindi cha Rauka ambacho alikuwa akiongoza kabla ya kuondoka zake kwenda Marekani.
Atakuwa anashirikiana na mcheza santuri Gee Gee na mwanamuziki wa injili ambaye pia ni mtangazaji, Timeless Noel.