Mwanzilishi mwenza wa lebo ya WCB Wasafi Babu Tale amewashangaza wengi baada ya kumtambulisha mwanawe ambaye hajawahi kuonekana kabisa.
Kupitia Instagram yake, Babu Tale alipakia picha ya wanawe wa kiume watatu ambao wengi wanawajua kutokana na ukawaida wake wa kuwapakia. Ila kweney picha hiyo pia palionekana sura mgeni ya binti mdogo ambaye mbunge huyo wa Morogoro Kusini alisema pia ni mwanawe kutoka kwa mwanamke mwingine.
Itakumbukwa mke wake Babu Tale alifariki yapata miaka miwili iliyopita na ilijulikana kuwa alimuacha na watoto watatu.
Jana pia mwanasiasa huyo akipakia picha hiyo alidokeza kuwa pia binti yake huyo ambaye ni sura mpya kabisa katika familia yake pia alimpoteza mamake miezi miwili iliyopita.
“Najua wengi wenu mtajiuliza huyu mwengine ni nani? Sababu hao watatu sura zao sio ngeni sana machoni mwenu. Huyo mgeni kwenu anaitwa ZAHID. Nimwanangu pia. Kama ilivyo hao watatu. Huyu nae nimempoteza mamayake miez miwili iliyopita,” Babu Tale alidokeza na kuwaacha wengi katika hali ya sintofahamu.
Hii sasa ni mara ya pili mwanasiasa huyo kumpoteza mwenza wake chini ya miaka miwili na alisema kwamba licha ya matokeo hayo yote bado anazidi kumuaminia Mungu kwa majaribio hayo kwani anaona kama anayamudu.
“Sina budi kumshukuru Mungu kwakila Mtihani anaonipa. Kwamaana anaamini nitauweza. Siwezi tena kulia,zaidi nakuomba uendelee kunifungulia riziki kila uchwao,” Babu Tale aliomboleza.
Vile vile alidokeza wazo la kuoa kwa mara nyingine tena huku akimuomba Mungu kumletea mwanamke mwningine atakayeshirikiana naye kuwalea watoto hao wanne sasa.
“Na naamini unaniandalia Mama yao mpya (mke mzuri) wa kuja kuwalea na kuwaongoza Kwenye misingi mizuri yakumjua Mungu,” alisema.
Watu wengi kando na kushangazwa na taarifa za kifo cha mkewe wa pili yapata miezi miwili iliyopita, ila pia walimzomea kwa kile walisema kwamba licha ya kuwa na mkewe wa kwanza bado alikuwa anachepuka mpaka kupata mtoto nje ya ndoa huku mkewe wa kwanza akiwa bado yupo hai.