Grace Sugut Kipchoge, mke wa bingwa mara mbili wa Berlin Marathon Eliud Kipchoge, amefichua kwamba alifunga kwa siku saba na kuomba miujiza ifanyike kwa mumewe katika mbio hizo.
Grace akizungumza na Jarida la Nation alisema alifuatilia mumewe akivunja rekodi nyumbani kwao katika eneo la Elgon View, Kaunti ya Uasin Gishu pamoja na familia yake pamoja na majirani.
Alisema kuwa alijawa na tabasamu usoni kuona ombi lake lilitimia.
“Nampongeza mume wangu kwa kuweka historia tena kwa kupunguza rekodi yake ya dunia. Nilikuwa katika hali ya maombi kwa wiki moja iliyopita na nilifunga ili muujiza utokee. Nina furaha kwamba ushindi umekuja nyumbani,” Grace alieleza jarida hilo.
Wakufunzi wa Kipchoge na mashabiki waliofuatilia mbio hizo kwenye runinga katika Mkahawa mmoja mjini Eldoret walisema mwanaraidha huyo alipovunja rekodi ya dunia kwa mara nyingine, walilipuka kwa furaha.
Kipchoge mwenye umri wa miaka 37, alitumia masaa mawili, dakika moja na sekunde tisa kushinda, na kuvunja rekodi yake ya awali ya rekodi ya dunia ya saa 2:01:39 aliposhinda Berlin mwaka wa 2018.
Kipchoge alimshinda mwenzake kutoka Kenya Mark Korir, aliyemaliza wa pili kwa muda wa 2:05:58 huku Tadu Abake kutoka Ethiopia akimaliza wa tatu kwa saa 2:06:28.
"Bado ninahisi mchanga, nikifikiria busara na mwili bado unachukua mafunzo'' Kipchoge alisema baada ya kushinda.
Licha ya hayo, Bingwa Eliud Kipchoge alitia kibindoni shilingi milioni 13.9 kwa kuivunja rekodi yake ya dunia katika mbio za marathoni za Berlin.
Kipchoge alitwaa karibu Ksh3 milioni kwa kushinda mbio hizo, Ksh6.8 milioni kwa kuvunja rekodi ya dunia na Ksh4.1 milioni kwa nyongeza ya muda.