Baada ya Pasta Ezekiel Odero kutoa mchango wa shilingi milioni 14.6 za Kenya katika mkutano wa maombi wa mwinjilisti Benny Hinn, sasa mchungaji mwenza, James Ng’ang’a naye amemtaka Ezekiel kumpa ‘kitu kidogo’.
Katika video ambayo imeibuka mitandaoni, Ng’ang’a alikuwa akizungumza kwenye kamera ambapo alifichua kwamba wachungaji wote kwenye mkutano huo waliombwa kuchangia kiasi cha pesa kwa ajili ya kuendesha shughuli zote.
Lakini alishangaa Ezekiel alipotoa kiasi Zaidi ya mara kumi na kile walichotakiwa kutoa, na hivyo kumuomba mchungaji huyo mkwasi kutoka kanisa la New Life Prayer Centre kumpa angalau kiasi kidogo pia.
“Ezekiel basi si unitumue kanusu. Ezekiel nitumie 10% ya hiyo…ama nitumie 50%... ama nitumie tu milioni 2 pekee. Kama uko connected na ufalme wa Mungu, utasikia vizuri kusapoti ufalme huo,” Pasta Ng’ang’a alisema.
Alikwenda mbele kusema kwamba mwinjilisti wa Marekani mwenye asili ya Israeli, Benny Hinn hakujua dola laki moja ni pesa kwamba katika sarafu ya Kenya.
Pasta Ezekiel alituma mwakilishi wake kutoa taarifa kwa Benny Hinn kwamba alikuwa radhi kutoa dola laki moja, lakini Ng’ang’a anasema Hinn alifikiria ni elfu 10 za kenya kumbe ni mamilioni ya Pesa zikibadilishwa kwenye sarafu za Kenya.
Mchungaji huyo wa Neno Evangelism alisema kwamba Hinn aliwataka wachunaji kila mmoja kutoa dola 10,000 akifikiria ni pesa ndogo, lakini baadhi ya wahubiri walitoroka baada ya kugundua kwamba walitakiwa kuchangia hiyo $10,000 ambayo ni milioni 1.5 za Kenya.
"Yeye (Benny Hinn) hakujua thamani ya dola 10,000 nchini Kenya. Waliokwenda huko walidhani ni KSh 10,000 za hustler. Ilipofafanuliwa (wachungaji) walirudi! Sio kama Benny Hinn hana pesa. ." Ng’ang’a alisema akicheka.