Chingiboy Mstado, meneja wa msanii Stevo Simple Boy amethibitisha kusitisha uhusiano wa kikazi na msanii huyo kutokana na kile alikitaja kuwa mazingira magumu ya kazi.
Katika mahojiano ya kipekee kwa njia ya simu na Moses Sagwe wa Radio Jambo, Chingiboy Mstado, ambaye kando na meneja pia ni msanii wa kujitegemea, alisema sasa atawekeza nguvu Zaidi katika kujiendeleza kibinafsi.
Msanii huyo alifichua kwamba imekuwa vigumu kufanya kazi na Stevo Simple Boy na akaona uamuzi bora wa kila mmoja wao ni kutengana, akisema pia kwamba uamuzi huo ulitokana na yeye kutotaka kujitumbukiza kwenye dimbwi la msongo wa mawazo.
“Ni kweli nimeshamuacha, sitaki nife kwa depression,” Chingiboy alithibitisha madai ambayo yamekuwa yakienezwa mitandaoni kuhusu utendakazi wao.
Alisema kwamba lengo lake baada ya kuachana na Stevo ni kujisukuma mwenyewe ili kumsaidia mamake.
“Sasa hivi kwa kifupi sifanyi kazi na yeye [Stevo Simple Boy], kwa sasa nataka nijisukume kwa bidii nipate kumsaidia mamangu,” aliongeza Mstado.
Akizungumzia madai ya msanii huyo kufukuzwa katika makazi alikokuwa akiishi sehemu za Buruburu na kurejea mtaa duni wa Kibera, Chingiboy alithibitisha kwamba ni kweli amerejea Kibera lakini akakanusha kwamba Stevo hakufukuzwa.
Chingiboy Mstado na msanii wake Stevo Simple Boy wamekuwa na uhusiano wa vuguvugu katika kipindi cha siku za hivi karibuni kutokana na mazingira magumu ya kufanya kazi ambayo meneja huyo alidai yanasababishwa na watu wanaomzunguka Stevo.