Esther Musila, mke wa msanii wa injili Guardian Angel amefichua sababu kuu ambazo anahisi zilichangia yeye kukosa kufurahia ndoa yake ya kwanza.
Akizungumza kwenye podikasti yake wakiwa na mumewe, Musila alisema kwamba anafurahia kuitwa mke katika ndoa ya sasa na msanii huyo kinyume na alivyokuwa akihisi miaka kadhaa iliyopita katika ndoa yake ya kwanza.
Musila alimpa hongera na pongezi Guardian Angel kwa kumfanya kufurahia kuitwa mke, hali ambayo hakuwahi kuihisi pengine kutokana na kuolewa akiwa bado mdogo.
“Na nikizungumza kutoka kwa nafsi yangu mimi kama mimi, na hiki ni kitu ambacho nimekuwa nikijisemea mwenyewe, niko katika wakati kwenye maisha yangu ambapo sasa ninaelewa ni nini maana ya kuolewa.”
“Pengine katika ndoa yangu ya awali, niliolewa nikiwa bado mdogo na hivyo sikupata nafasi ya kufurahia kuwa mke. Pengine kwa sababu sikupatiwa ile fursa. Nilikuwa mdogo, nikapata watoto ningali bado mdogo, kwa hiyo ilikuwa Zaidi kuhusu watu wengine. Lakini sasa ninafurahia kuwa mke, na kuchukuliwa kama mke, kwa hiyo pongezi kwako,” Musila alimwambia Guradian Angel.
Kwa upande wake, Guradian Angel alisema kwamba ndoa imemkuza pakubwa kiasi kwamba amejikuta kuwa mwanamume wa kuwajibika.
“Kwangu nafikiri ndoa imenikuza, hata katika kiwango cha kukomaa kwangu binafsi, nidhamu yangu, kujua kwamba siwezi rauka asubuhi na kufanya vitu jinsi ninavyotaka, hiyo pia ni nidhamu kivyake ukizingatia kwamba kabla ya ndoa nilikuwa na maisha huru, na nafikiri wengi wrtu hujifunza kutoka kwa nafasi ya kuwajibika,” Guardian Angel alisema.
“Ukiangalia maisha yangu ya sasa na ulinganishe na maisha yangu ya awali, nilikuwa mwenye talanta kubwa, nilikuwa nafanya muziki mzuri – ambayo ni sehemu ya sababu tuko pamoja – lakini kuna baadhi ya vitu ambavyo havikuwa bado vimefanyika katika maisha yangu. Baadhi ya vitu havikuwa vimefunguka kabisa kwa sababu sikuwa na wewe, au sikuwa ninawajibika kwa mtu mwingine. Kutoka kwa upande wa kukomaa, ni pahali pazuri kukuwa. Kuwajibika,” Guardian Angel aliongeza.