Taarifa za kifo chake zilitangazwa kwenye mitandao ya kijamii na waigizaji wenzake ambao walifichua kwamba mzee huyo alifariki katika hospitali ya Temeke jijini Dar es Salaam alikokuwa amelazwa kwa matibabu.
Kwa wale wasiomfahamu Mzee PEMBE, ni mchekeshaji aliyempa umaarufu wa kudumu msanii Aslay kipindi anaanza kuimba akiwa tineja.
Alsya alimtumia mzee huyo kuigiza kama baba yake katika video ya wimbo wake wa 'Nakusemea kwa mama' ambao ulipaisha kipaji cha dogo huyo akiwa chini ya Mkubwa na Wanawe.
Ni mzee ambaye katika harakati zake za kisanii, alipenda sana kutembea na rungu moja kubwa ajabu.
Aslay kupitia instagram yake, alimuomboleza mzee huyo na kumtaja kama mtu aliyefungua barabara yake katika maisha ya muziki na sanaa.
"Moja kati ya watu walionifungulia na kunitengenezea barabara yangu ya maisha na muziki ni huyu mzee PEMBE. Nimepokea kwa masikitiko makubwa kwa kifo chake. Mungu ailaze roho yake marehemu mzee wetu Pembe mahali pema peponi. Pole ziwaendee familia yake na wapenda burudani wote," Aslay aliandika kupitia Instagram yake.
Baadhi ya mashabiki wa muziki wa msanii huyo walikiri kumfahamu mzee huyo kupitia wimbo wake wa kwanza.
"Niliposikia taarifa za kifo chake nilikumbuka wimbo huu," alisema mchekeshaji wa Kenya, Dj Shiti.
"Duuh, hii nyimbo nilikuwa naipenda kinomanoma kwa kweli, kwa sababu ya huyu mzee PEMBE," alisema mwingine.
Waigizaji wenzake kama Mau Fundi na Vincent Kigosi walifichua kwamba mzee PEMBE amekuwa akiugua kwa muda hospitalini ambapo alikuwa anaumwa sana.
Mzee huyo alizikwa Jumatatu nyumbani kwake kuambatana na mila na desturi za dini ya Kiislamu.