Msanii anayetajwa kuwa nambari moja katika miziki ya injili ya kizazi kipya humu nchini, Guardian Angel amesisitiza kwamba yeye ndiye alikuwa wa kwanza kumpenda Esther Musila na si vinginevyo.
Akizungumza kwenye klipu ambayo aliichapisha kwenye chaneli yake ya YouTube, Guardian Angel alifichua kwamba safari yao ya mapenzi ilianza wakati wa ujio wa janga la Covid-19.
Msanii huyo anayetamba kwa jina la majazi la ‘Gospo 1’ alieleza kwamba Musila alikuja katika maisha yake kumpa msaada wa kumuinua kimuziki, lakini yeye akataka vcitu vingine ambavyo bila shaka alivipata hatimaye.
“Mke wangu aliniaminia hata kabla uhusiano wetu kuanza. Alikuwa na shauku kuu ya kunisaidia na kuniunga mkono nitoboe kimuziki. Na kupitia kwake kutaka kunisaidia, nilizama katika mapenzi, nikataka vitu tofauti na nikapata,” Guardian alisema huku akicheka.
Msanii huyo ambaye alifanya harusi na Musila mapema 2022 alisema kwamba wakiangalia maisha yao pamoja miaka 3 baadae, anahisi kwamba kila mmoja wao amepata na kuridhika na kile ambacho alikuwa anafukuzia katika maisha.
“Leo hii mimi na mke wangu kila mmoja amepata chenye alikuwa anataka, kwa sababu yeye alipata kunisaidia kufika pahali alitaka nifike na mimi nilipata mapenzi, na nikapata mke na maisha fiti.”
Guardian Angel na Esther Musila walioana na kuvutia hisia mseto miongoni mwa Wakenya ambao walihisi kwamba msanii huyo alipotoka kutoka kimapenzi na mwanamke mwenye umri mkubwa mara dufu kumshinda.
Guardian anaaminika kuwa na umri wa miaka 34 wakati Musila ana umri wa miaka 54 na wameishi pamoja kwa zaidi ya miaka 3 sasa.