MCHUNGAJI
wa kanisa la
Neno Evangelism, James Maina Ng’ang’a ameonya waumini dhidi ya matumizi ya
kauli tata ambazo zimeibukia mitaani.
Akizungumza katika moja
ya ibada zake Jumapili iliyopita, Ng’ang’a alisema kwamba kauli hizo ambazo
zinatumiwa na vijana wengi si za kufurahisha kwa macho na maskio ya waumini,
akitoa onyo kali dhidi ya matumizi yake.
Mchungaji huyo alisema
kwamba kauli kama ‘Anguka Nayo’ iliyoibuka miezi michache iliyopita na ile ya ‘Mapangale’
ambayo imewagawanya watumizi wa mitandao ya kijamii katika kipindi cha wiki
moja iliyopita ni kauli potofu zisizo na nafasi hata kidogo katika maisha ya
walio okoka.
“Hizi lugha zimetokea
wewe uliyeokoka usizizungumze. Maana zimekuja lugha zenye zina ushetani. Hayo
maneno wanaita sio hivyo, hizo nyimbo, sikiliza… kuna mmoja aliniambia eti
anguka nayo. Hiyo ni yao. Alisema hiyo sijui na gani inaitwa ‘panga panga’ ni
yao hiyo,” Ngang’a alisema.
Aliwashauri waumini wake
na haswa wale ambao wanazimia kuja kuwa wahubiri kutochochewa na kauli kama
hizo akisema kwamba ni heri wasizikubali kabisa katika mihadhara yao ya injili.
Mchungaji Ng’ang’a
alisema kwamba kauli kama hizo ni za sajili ya kwenye vilabu vya starehe na
wala si kwenye mikutano ya injili kama kanisani.
“Wale ambao mtakuja kuwa
wahubiri, mkuwe makini na kusema hii hamtaimba hapa kanisani, nendeni mkaimbe
huko kwa baa. Hamtaimba hizo nyimbo hapa,”
Ng’ang’a alisema.
Mchungaji huyo alitoa
kauli hiyo ikiwa ni wakati ambapo watumizi wa mitandao ya kijamii wamegawanyika
katika matumizi ya kauli hizo mitaani.
Wiki iliyopita,
mitandaoni kulikuwa na mjadala mkali kuhusu kauli ya ‘Mapangale’ ambayo
ilibuniwa siku chache zilizopita.
Watu walikuwa wanajadili
matumizi ya kauli hiyo ambayo iliasisiwa na mshereheshaji Zendiambo, wakisema
kwamba ilikuwa inaunga mkono visa vya mauaji ya wanawake ambayo yamekithiri
humu nchini.
Hata hivyo, Zendiambo
alijitokeza na kutetea ‘mapangale’ dhidi ya madai hayo akisema kwamba ni kauli
ya mtindo wa kucheza densi vilabuni tu.
Aidha, alisema kwamba
hakuna aliyeshrutishwa kuitumia, akiwataka wale wanaohisi ni ya uchochezi
kuiacha kwa matumizi ya wale wanaoielewa.
Mjadala kuhusu uhalali
wa kauli hiyo unajiri wakati ambapo mauaji dhidi ya wanawake limekuwa ni kero
humu nchini katika miezi ya hivi karibuni, baadhi ya watu wakiitaka serikali
kutangaza mauaji dhidi ya wanawake kuwa janga la kitaifa.
Kwa upande mwingine,
kauli ya ‘Anguka Nayo’ ilipata mwamko wa kipekee wakati wa maandamano ya vinana
wa Gen Z dhidi ya mswada wa kifedha wa mwaka 2024.
Shinikizo la maandamano
ya wiki kadhaa liliona rais Ruto akiufutilia mbali mswada huo, katika kile
vijana walisema kwamba amelazimika ‘kuanguka’ na mswada huo.
Kauli hii iliwachochea
vijana wanamuziki wa kundi la Wadagliz kuachia wimbo ‘Anguka Nayo’ ambao
uliwavutia wengi na kuufanya kuwa kibwagizo cha kila sehemu.
Kilele cha umaarufu wa
wimbo huo uliwapa vijana hao nafasi adimu ya kumtumbuizia rais na wageni wake
katika uwanja wa Kwale wakati wa sherehe za kuadhimisha siku ya mashujaa mnamo
Oktoba 20.