Gavana wa kaunti ya Nairobi Johnson Sakaja ameahidi kutaja baadhi ya barabara katika kaunti anayoongoza majina ya wasanii tajika waliovuma kama njia moja ya kuwakumbuka kwajuhudi zao za kuweka msingi bora katika sekta ya usanii nchini.
Gavana huyo alisema hayo katika maadhimisho ya miaka 61 ya Jamhuri iliyoandaliwa ugani Uhuru Gardens jijini Nairobi mnamo Alhamisi gavana Sakaja akiahidi kuipa barabara moja katika mtaa wa South C jina E-Sir ambaye alikuwa msaani tajika wa rap nchini.
‘’Nimeongea na mwenzangu mheshimiwa Jalas na tutabadilisha majina ya baadhi ya barabara jijini na kuzipatia majina ya wasanii wetu mashuhuru. Barabara iliyo katika eneo la South C itapewa jina la E-Sir na hata ndugu yake ametutumbuiza hapa kama njia ya kuwakumbuka na kuwapa heshima wasanii wetu mashuhuri,’’ Alisema Sakaja.
Msanii tajika nchini David Mathenge maarufu kama Nameless alimtaka gavana Sakaja kuita barabara moja jijini Nairobi jina la E-Sir kwa kumbukumbu za msanii huo kutokana na mchnango wa kimziki aliokuwa nao.
Nameless aliyekuwa pamoja na E-Sir wakati wa ajali iliyomwangamiza, alianza mchakato wa kukusanya sahihi katika mtandao na kufanikiwa kupata maelfu ya sahihi wakati huo na sasa ombi lake linaonekana kutimia baada ya hotuba ya gavana Sakaja kwenye sherehe za Jamhuri Dei Disemba 12, 2024.
E-Sir aliyejulikana kwa jina lake halisi kama Issah Mmari alifariki tarehe 16 Machi 2003 kwenye ajali ya barabarani akielekea Nairobi baada ya kutumbuiza mashabiki kwenye tamasha lililofanyika katika sehemu moja ya burudani jijini Nakuru.
Baadhi ya ngoma zake zilizotamba ni pamoja na ‘Leo ni Leo’ na ‘Moss Moss’ ambazo bado zinazidi kutamba miaka kadhaa baada ya kifo chake.