Mke wa mwimbaji Guardian Angel Esther Musila amemsherehekea marehemu babake huku akioadhimisha miaka kumi na miwili tangu mzazi huyo wake afariki.
Katika taarifa yake ya Jumamosi, Esther alisema kwamba baba yake alikufa siku kama hiyo miaka kumi na mbili iliyopita na akataka roho yake iendelee kupumzika kwa amani.
Pia alimtaka marehemu babake awe na amani kwani anaamini aliungana na mama yao mbinguni.
“Baba, leo unatimiza miaka 12 tangu uende kuwa na Bwana. Endelea kupumzika kwa amani kwani tunajua wewe na mama mmeungana mbinguni,” Esther alisema.
Aliambatanisha taarifa yake na picha ya kumbukumbu ya marehemu baba yake.
Babake Esther Musila alipoteza maisha mnamo Desemba 2012. Alikuwa na umri wa miaka 73 alipofariki.
Miaka michache baadaye, mke huyo wa Guardian Angel alibaki kuwa yatima kwani kwa bahati mbaya mamake pia aliaga dunia.
Mwaka jana, Bi Musila alimkumbuka marehemu mamake takriban miaka saba baada ya kuaga dunia.
Wakati akimsherehekea mzazi huyo wake, Bi Musila alimtaja marehemu kama nguzo kuu ya maisha yake.
"Ulinifundisha kuthamini kila siku ya maisha yangu na kuishi kana kwamba hakuna kesho. Nililelewa na mwanamke mwenye nguvu na najua kila wakati ulikuwa unasimama nami," alisema kwenye mtandao wa Instagram.
Musila alimuombea mzazi huyo wake mapumziko ya amani na kueleza jinsi anavyojivunia miaka ambayo walishiriki pamoja.
Hata hivyo, alieleza anavyotamani marehemu angekuwa hai ili ashuhudie maendeleo yake na akutane na mumewe Guardian Angel.
"Mama, natamani ungeishi muda mrefu zaidi ili ukutane na mwanaume mzuri zaidi katika maisha yangu sasa. Najua ungefurahi sana kuniona katika nafasi hii mpya na najua tungekuwa tukiimba nyimbo uzipendazo pamoja," alisema.
Aliongeza,"Wajukuu zako pia
wamefanya upate fahari kama vile ungetaka wafanye. Endelea kutuangalia sote
hadi siku moja tutakapokutana tena. Tunakukumbuka na tunakupenda milele
mama."
Musila alifichua kuwa mama yake alifariki akiwa usingizini, saa chache tu baada ya yeye na kaka yake kumtembelea.
Alitaja siku ambayo mamake alifariki kama siku ya giza zaidi maishani mwake huku akisimulia matukio yaliyofuata.
"Miaka 7 iliyopita, asubuhi kama hii, nilipokea simu kwamba mama yangu mpendwa amefariki usingizini. Hii ilikuwa chini ya saa 12 baada ya mimi na kaka yangu Fred kwenda kijijini kwa wikendi. Ilikuwa siku mbaya zaidi katika maisha yetu."
"Bado sijui tulipataje nguvu ya
kuendesha gari hadi Machakos, kwa kweli ilionekana kama ndoto. Ninaamini kabisa
hadi leo kwamba Mwenyezi alilisuluhisha kwa njia yake mwenyewe na alitaka
tutumie saa za mwisho za maisha ya mama pamoja naye," alisema.
Esther Musila alizaliwa Machakos yapata miaka 54 iliyopita na yeye ndiye mtoto wa kwanza kuzaliwa na binti pekee wa wazazi wake.