MSANII wa kizazi kipya wa humu nchini Otile Brown amedokeza uwezekano wake kuchukua likizo kutoka katika mitandao ya kijamii mwaka huu.
Kupitia Instagram, Otile Brown alifichua kwamba kila
wakati anapoingia katika mitandao ya kijamii, anajawa huzuni mwingi kutokana na
jinsi mambo ya kisiasa yanavyotendeka.
Msanii uyo ambaye katika siku za hivi karibuni
amekuwa katika mstari wa mbele kuikashifu serikali kutokana na kukithiri kwa
visa vya utekaji nyara wa vijana kadhaa alisema kwamba kila wakati anapata
huzuni mwingi kwa sababu ya nchi yake – Kenya.
Brown alisema kwamba kutokana na hilo, huenda
akatatmini kuchukua likizo ya muda kutoka kwa mitandao, akisema kwamba roo yake
iko huru hata kama mwili wake utachukuliwa.
“Nina
huzuni kila dakika nyingine kwa sababu ya nchi yangu. Siwezi kujizuia, nadhani
ninafaa kukaa nje ya mitandao ya kijamii kwa dakika moja. Chukua mwili wangu
lakini roho yangu iko huru,” Otile Brown aliandika.
Kauli yake inajiri wiki moja tu baada ya kutoa kauli
nyingine ya kuonya serikali dhidi ya kuendelea kuwapuuza vijana na matakwa yao.
Brown alisema kwamba imekuwa kama kawaida kwa
viongozi kuona vijana kama watoto wa kuchezea shere, lakini akaonya kuwa upo
wakati vijana watasema imetosha na kuamua kuchukua sheria mikononi.
“Viongozi
wetu kuchochewa na vijana kwenye mitandao ya kijamii ni jambo la kushangaza
sana. Unatarajia nini ukikataa kuwawezesha? Utafika wakati hawatakuwa na
chochote ca kupoteza. Huku nje ni kugumu, nyinyi [viongozi] hamwezi kuelewa
hisia ya mtu asiye na chochote cha kujivunia hata baada ya kufanya kila kitu
kizuri masomoni,” Otile Brown alisema Desemba 28 kupitia instagram.
Alijiunga na vijana wengine mitandaoni ambao wamekuwa
wakishinikiza kutaka kujua waliko baadhi ya vijana wanaharakati ambao
waliripotiwa kutoweka baada ya ku8tekwa nyara wiki 2 zilizopita.
Hata hivyo, baadhi ya vijana hao wameripotiwa
kuachiliwa na kuungana na familia zao mapema Jumatatu asubuhi.