LILLIAN Ng’ang’a amejipanda kwenye mgororo wa matusi na watumizi wa mitandao wa X baada ya kutoa rai kwa watumizi wa mitandao ya kijamii kuwakosoa viongozi kwa njia ya heshima.
Katika chapisho lake ambalo lilivutia kauli nyinjgi
za matusi, mama huyo wa mtoto mmoja alisema kwamba watu wengi wameifanya kuwa
kawaida kuwakosoa viongozi mitandaoni kwa kutumia lugha ya matusi.
Kwa mujibu wa Ng’ang’a, kuwakosoa viongozi kwa
kutumia lugha ya matusi kunayeyusha maana halisi ya ukosoaji, na kuwataka
kutumia lugha ya heshima katika ukosoaji wao.
“Kutumia
lugha chafu na kutowaheshimu wengine si jambo la lazima, kwa kadiri tunavyopaswa
kuwawajibisha viongozi wetu. Sambaza ujumbe wako kwa njia ya ukomavu, yenye
heshima. Kuongeza matusi kunapunguza kusudi,”
Lillian Ng’ang’a alirai watu.
Hata hivyo, rai yake ilipokelewa kwa njia hasi na
watumizi wa mitandao huo wa X, baadhi wakilivuta jina lake na kuliburura kwenye
matope wakidai kwamba amenunuliwa na viongozi.
Vuta-nikuvute hii inajiri wakati ambapo baadhi ya
viongozi haswa wale walioko serikalini wamekuwa wakichuana kwa maneno makali ya
watumizi wa mitandao ya kijamii, kwa kile viongozi hao wanadai kwamba vijana
wamepotoka kimaadili.
Rais Ruto, ambaye amekuwa mwathirika mkubwa wa hulka
ya vijana mtandaoni kumtupia maneno na kauli za kudhalilisha uongozi wake
amekuwa akitoa rai kwa wazazi mara si moja, akitaka wazazi kuwapa wanao mafunzo
ya maadili mema.
Kwa upande mwingine, waziri mpya wa masuala ya ndani
Kipchumba Murkomen ametema moto kwa vijana wanaotumia mitandao ya kijamii
kuwadhalilisha viongozi kwamba sheria itawavizia.
Murkomen alisema kwamba si kupotoka kimaadili kwa
hali ya juu kwa mtu kutumia utandawazi wa AI kubuni picha bandia ya kiongozi
akiwa kwenye jeneza.
Alisema tabia hiyo si ya kufurahikiwa, huku akiwasuta
wazazi na viongozi wa kidini kwa kuwakingia kifua wale wanaofanya hivyo.