KHADIJA Kopa, mamake msanii kutoka WCB Wasafi, Zuchu amekuwa mtu wa hivi punde kutia neno kuhusu zogo linaloendelea baina ya mwanawe na chombo cha Habari cha Wasafi FM lakini pia na bosi wake Diamond Platnumz.
Kopa alizungumza na waandishi wa Habari wakati
wa mkutano wa chama tawala Tanzania, CCM ambapo aliweka wazi kwamba mwanawe
Zuchu muda ukifika atapata tu mwanamume sahihi wa kumuoa.
Hii ni baada ya Diamond
kuonekana akikana kuwa na mahusiano ya kimapenzi na Zuchu kwenye kipindi cha
Netflix, licha ya kudai kuwa mpenzi wake kwa miaka 3 sasa.
Khadija Kopa alisema
kwamba hajasema kama Diamond atamuoa mwanawe na kusisitiza kuwa Zuchu bado
hajachelewa kupata mpenzi sahihi wa kufunga ndoa naye.
“Haditih za sijui
mwanangu aolewi hazinikwazi kwa sababu sio mimi ndio naolewa. Pia sio mimi ndio
niliyemwambia mtu muoe. Hayo ni mambo ya kawaida tu, ikifika siku ataolewa. Na mimi
sijasema DIAMOND, nimesema muda ukifika Mungu akimjaalia atapata mume atamuoa,”
mama Kopa alisema.
Kopa alitaja sekeseke za
Diamond na Zuchu kama upuzi ambao hana muda wa kushughulika nao.
“Mimi sishughuliki na
upuzi wao, mimi nashughulika na mambo yangu tu. Hayo mambo hata msiniulize,”
Khadija Kopa alisema.
Kauli hizi zinajiri siku
chache tu baada ya Diamond kuonekana kumdhalilisha Zuchu kwa kumkana bayana
kwenye tamthilia ya Young, Famous & African iliyotoka mwishoni mwa juma
lililopita.
Hata hivyo, Diamond
kwenye mitandao ya kijamii aliwataka mashabiki kuacha kumfitinisha na Zuchu
akijitetea kwamba ule ni mchezo tu kwenye tamthilia na wala si kila kitu
alichokiigiza pale kinamaanisha ukweli katika maisha yake ya uhalisia na Zuchu.
Msanii huyo alisema
kwamba anambeza sana Zuchu na kuonyesha kwamba bado anampenda licha ya kuwa
tofauti kwenye Netflix.
Zuchu na mtangazaji wa
Wasafi, Juma Lokole wiki jana walizua mtafaruku mkali kwenye Instagram, baada
ya Lokole kumtaja kuwa king’ang’anizi anayelazimisha ndoa kwa Diamond.
Kauli hiyo ilimkera
Zuchu ambaye alifuta utambulisho wa WCB Wasafi kwenye bio yake Instagram na
hata kutishia kuivuta lebo hiyo mahakamani kwa kudai kwamba ananyanyazwa.