MSANII aliyejizolea umaarufu miaka ya 2010s kutokana na nyimbo zake za injili haswa kwa lugha ya Kimaasai, L-Jay Maasai amerudi upya katika tasnia ya injili.
Maasai ambaye amekuwa akipitia changamoto nyingi za
maisha tangu mwaka 2022 alikwenda kimya lakini amefanya ujio wa kishindo katika
injili ya Kimaasai na wimbo wake mpya ‘Ashomi Shomo’ – tafsiri yake kukutana na
Yesu.
Akisimulia ujio wake baada ya muda mrefu wa
changamoto za kimaisha zilizomsababishia msongo wa mawazo mwaka 2022, L-Jay
Maasai amefichua kwamba amezaliwa upya na kuanza maisha mapya katika kanisa la Enlightened Christ Embassy –
ECE.
“Ninapoanza safari mpya na kutembea na Kristo , Huyu ndiye "MWANA WA UDONGO" aliyezaliwa mara ya pili, aliyerejeshwa na kurekebishwa katika Kanisa la Enlightened Christ Embassy Church (ECE). Chini ya uangalizi mzuri na mwongozo wa Baba yangu Nabii, Brian Omondi,” Maasai alisema.
Msanii huyo alifafanua msukumo wake wa kuandikwa wimbo
wa Ashomi Shomo akisema kwamba ni kuzingatia simulizi ya kweli ya maisha ambayo
ameyapitia katika miaka ya hivi karibuni alipozama kwenye msongo wa mawazo.
“Imekuwa
safari, iliyojaa taabu na mitego, haikuwa rahisi kushinda changamoto na
kupigana kupitia vita lakini leo, ninasimama kama shahidi na ninaweza
kushuhudia kwa fahari rehema, kibali na baraka za Mungu. Hakika Yeye ni
mwaminifu.”
“Kuhusiana
na hili Nawaleteeni "Ashomi Shomi" wimbo unazungumzia vita yangu ya
muda mrefu ya mambo ya kidunia" yaliyojaa Unyogovu na kushindwa licha ya
kuwa LJay Maasai. Ni utambuzi kwamba tunaweza tu kuamini na kukaa chini ya
mbawa za Mungu, haijalishi. kile ambacho maisha yanatupa kwa sababu Yeye ni
Mwaminifu, mwadilifu na Mungu wa nafasi ya Pili Yeremia:29;,”
alifafanua.
Masaibu ya L-Jay Maasai yalifahamika wazi kwenye
jamii ya mitandao ya kijamii Februari 2022 alipojitosa kwenye Facebook na kuandikwa
barua ndefu akisimulia alivyokuwa anateseka na kuumia maishani licha ya
kujijengea jina la kibabe kwenye sanaa ya muziki wa injili.
Katika barua hiyo ya kumlalamikia mkewe, Msanii huyo
alisimulia kwa uchungu jinsi familia yake ilisambaratika baada ya mkewe
kumuacha na kumzamisha zaidi kwenye lindi la mawazo yasiyojua kupoa.
“Ninaamini unajua mpenzi wangu kwamba
nimeumia sana na nimesumbuliwa mno na msongo wa mawazo, wasiwasi, mafadhaiko na
unyongovu, mpaka nimefikiwa kiwango ninakosa ladha hata katika Maisha yenyewe.
Muda mwingine nimefika mahali mpaka nafikiria kujiuwa. Kwa kifupi, ninahisi nimepoteza
maana katika dunia hii,” sehemu ya ujumbe huo mrefu ilisoma.
Maasai pia alizidi kujieleza katika barua
hiyo na kumwambia aliyekuwa mkewe Flo Mutia ni kwa jinsi gani amembeza katika
Maisha yake kwamba katika kila jambo amekuwa akifanya, mkewe yuko katika mawazo
yake hata kama hakuwa anamuona kwa macho.
“Ni mengi ambayo naweza kuandika lakini siwezi hitimisha
barua hii bila kukuambia ni kwa jinsi gani nimekuwa nikiumia bila uwepo wako
maishani mwangu. Siku zote utabakia kuwa namba moja kwangu, haijalishi mahali
nitaenda, chenye nitafanya au chenye nitasema,” alifikia kikomo L-Jay Maasai.
Miaka 3 baadae, Maasai ameibuka kijasiri na kuandikwa tungo hiyo
ya Ashomi Shomo akisimulia kukutana na Yesu na kuanza ukurasa upya wa maisha.
Bila shaka, hii ni hatua ya kijasiri ambayo si wengi
wanaimudu kujikung’uta mavumbi na kuanza tena!