MFANYIBIASHARA na mtangazaji wa runinga, Betty Kyallo amewafunga midomo watu ambao wanakashifu penzi lake na mpenzi wake, Charliemny.
Kupitia ukurasa wake wa Instagram, Betty Kyallo alirundika picha akionyesha jinsi wikendi yake ilifana akiwa na mpenzi wake.
Katika picha hizo, wawili hao walionekana wakifurahia mandhari mazuri na Kyallo akawashauri wanaoonea gere penzi lao kutafuta mtu ambaye wanaweza cheza naye kitoto kama wao.
“Mimi tu na rafiki yangu bora tukizunguka. ❤️❤️ Tafuta mtu wa kuwa kama mtoto naye … Hisia nzuri zaidi. Wacha nijaribu kumuamsha😅 @charliemny I Love You,” Betty Kyallo alichapisha.
Kyallo amekuwa mtu wa kulitetea penzi lake bayana licha ya ukosoaji mkubwa kutoka kwa sehemu ya watumizi wa mitandao ya kijamii.
Kyallo aliweka wake kuhusu penzi lake na kijana huyo ambaye mwanzoni alikuwa anamficha kutotambuliwa na wanamitandao ya kijamii lakini kadri siku zilivyozidi kusonga, alijihami na ujasiri na kumtambulisha.
Baadhi walihisi Kyallo aliamua liwalo na liwe na kumweka kwenye mitandao ya kijamii baada ya baadhi kuibua dhana kwamba alikuwa anachumbiana na kijana mdogo zaidi kiumri.
Japo alikiri kwamba Charlie ni mdogo kiumri kumliko, lakini Kyallo alitetea penzi lake akisema kwamba ni mtu mzima mwenye uwezo wa kujifanyia maamuzi.
Akizungmza na Eric Omondi kwenye kipindi anachoongoza yeye kwenye runinga ya TV47 Mei mwaka jana, Kyallo alikanusha vikali uvumi kwamba mpenzi wake alikuwa ni wa umri wa miaka 21.
"Maneno mengi ambayo mnapata mitandaoni ni ya uongo, hiyo 21 ni uongo mtupu,” Kyallo alisema.
“Hata mpenzi wangu angekuwa 21 huyo bado ni mtu mzima, lakini umri wake si 21. Hebu tuache kuingia sana kuhusu hilo,” alisema.
Hata hivyo aliendelea kutania jinsi wazee wanavyochoshwa na kuonyesha upendo kwa kuwa wanashikiliwa na familia na masuala mengine.
“Tuliamua tuwapatie wazee muda wapumzike kidogo, unajua, wajishughulishe na mambo yao. Kuhusu harusi sisi tuko harusi kwa sasa, hiyo stori ya harusi na kupatiwa watu presha hapana, acha tu nishughulikiwe na mtoto wa wenyewe kwa sasa,” alisema.
Uvumi kuhusu uchumba wa Betty uliibuka baada ya kufichua katika kipindi chake cha Friday With Betty kwenye TV47 kwamba alikuwa kwenye uhusiano mzito na alifurahishwa sana.
“Mtu wangu anatoka kanda ya magharibi. Sasa nimetulia. Najisikia furaha,” Kyallo alieleza.