TIKTOKER Baba Talisha amemshambulia vikali nyanyake aliyekuwa TikToker Brian Chira kwa kile anadai kwamba bibi huyo hana shukrani.
Kupitia chapisho lenye aya ndefu kwenye ukurasa wake wa
Instagram, Fastine Lipuku Lukaale, maarufu kama Baba T alimzomea nyanyake Brian
Chira kwa kuendelea kuwataka TikTokers kumsaidia zaidi.
Kwa mujibu wa Baba Talisha, bibi huyo anafaa kuwa mwingi wa
fadhila kwa jamii ya TikTokers waliochanga zaidi ya Sh8m kumjengea nyumba
ambayo sasa anataka kuuza.
Baba Talisha alisema kwamba bibi huyo anafaa kuwa na shukrani
kwani hakuna mtu mwingine nchini amewahi changiwa kiasi hicho cha fedha, lakini
kwa mshangao wa wengi, anataka kusaidiwa zaidi.
"Ninahisi aibu kuona
mtu ambaye amesaidiwa na familia ya mtandaoni, haswa kwenye TikTok, akiwa hana
shukrani. Ksh8.4 milioni zilikusanywa. Ilisalia na Ksh7.4 milioni chini ya
mwaka mmoja kwenda chini, hakuna chochote. Hakuna mtu katika historia ya
uchangishaji ambaye amesaidiwa kama yeye. Ilikuwa haitoshi kwake,” Baba Talisha alieleza.
Nyumba inayozungumziwa inayojulikana kwa upendo kama
"Chira Clan," ilijengwa kama kumbukumbu kwa mtayarishaji maudhui
marehemu Brian Chira.
Kabla ya kifo chake cha kusikitisha, Chira alikuwa na ndoto
ya kuandaa nyumba nzuri kwa nyanya yake.
Kwa heshima ya ndoto yake, jamii ya TikTok ilikusanyika pamoja,
na kuchangisha Ksh8.4m ili kumjengea nyumba iliyo na samani kamili.
Mwaka mmoja baadae, nyanyake Chira ameibuka na madai kwamba
eneo iliko nyumba hiyo hakuna usalama wa kutosha na kuonyesha nia ya kutaka
kuiuza.
Bibi huyo alitoa wito kwa TikTokers kukaa chini ili
kumfikiria tena katika suala la usalama wake la sivyo atalipiga mnada jumba
hilo na kuhama.
“Sitauza vitu vyenu bila
ruhusa yenu. Nataka mkae chini muone shosho atakaa aje. Kama mtanijengea ua la
umeme ama kununua shamba na kunijengea mahali pengine. Kulikuwa na wezi hivi
majuzi na nilimpigia Obidan simu lakini hakupokea. Wanaiba ng’ombe na vitu
vingine. Hakuna usalama,” nyanyake Chira aliomba.
Suala hilo limeonekana kuwakera baadhi ya TikTokers, Baba
Talisha ambaye alikuwa mstari wa mbele kuchangisha fedha hizo akiwa wa hivi
punde kuvunja kimya chake.