ALIYEKUWA mke wa msanii Juliani, Lillian Nganga amewaziba midomo wale ambao wamekuwa wakimtupia maneno ya kila aina, siku chache tu baada ya kuweka wazi kwamba penzi lake na rapa huyo wa ‘Utawala’ lilizama.
Kupitia ukurasa wake wa X mnamo Machi 12,
Nganga alisema kwamba haoni sababu yoyote kwa watu kumrejelea kama mjinga
mitandaoni kisha kuvunjika kwa mahusiano yake ya kimapenzi.
Kwa mujibu wake, yeye haoni aibu yoyote
kuvunjika kwa mahusiano yake ya kimapenzi kwani amekuwa na wanaume wawili tu
tangu alipokuwa na umri wa miaka 25 hadi sasa anapoelekea miaka 40.
“Je, ukweli kwamba nimekuwa na
wanaume wawili tu tangu nikiwa na umri wa miaka 25 (ninatimiza miaka 40 mwaka
huu) unawezaje kunifanya mambo yote ya kipuuzi mnayoniita? 🤣
Pumbavu, Wajinga sana!” Lillian Nganga
alichapisha.
Akirejelea uhusiano wa zaidi ya miaka 10
na aliyekuwa gavana wa Machakos ambaye sasa ni Waziri wa leba Alfred Mutua
ambao ulivunjika mwaka 2021, Nganga alisema kwamba anajionea Fahari kuwa
miongoni mwa watu waliosimama na mwanasiasa huyo katika kampeni mara mbili na
kushinda ugavana naye.
Nganga aliyeonekana kusimama kidete pasi
na kutetereka dhidi ya mashambulizi kutoka kwa wanamitandao alisema kwamba huo
ni mwanzo tu na yeyote ambaye atashindwa kustahimili majibu yake basi ajiondoe
mapema kwenye gumzo.
“Nilikuwa na bahati ya kuendesha
chaguzi mbili na kushinda (jambo ambalo baadhi yenu hamtawahi kupata uzoefu),
kwa hivyo upende usipende, nitaendelea kushiriki maoni yangu kuhusu mambo
tofauti. Huu ni mwanzo tu. Chafua kubaki au kujiondoa,”
alisema.
Katika mahojiano ya kipekee na Dr
Ofweneke, mke wa gavana wa zamani wa Machakos na mwandishi alizungumza kwa
uwazi kuhusu mtazamo wake kuhusu mahusiano, akiweka wazi kuwa haamini
kushikilia wakati kitu kimeenda mkondo wake.
Alisema kwamba anapendelea kukumbatia
uzoefu, kuthamini masomo aliyojifunza, na kusonga mbele bila mapambano yasiyo
ya lazima.
"Sitatizika kushikilia tu kitu
wakati wakati wake umekwisha. Ninathamini kile tumekuwa nacho, kumbukumbu au
masomo, kisha tunaendelea tu,” Lillian
alishiriki, na hivyo kuonyesha kwamba hakuwa na majuto kuhusu mahusiano yake ya
zamani.