
KAMPUNI ya magari ya uchukuzi wa umma jijini Nairobi na Maeneo jirani, Metro Trans imetangaza kuandaa warsha ya kutoa mafunzo na hamasisho kwa madereva, makondakta na wafanyikazi wao wengine.
Kupitia machapisho kwenye kurasa zao za mitandao ya kijamii,
Metro Trans walitangaza kwamba hafla hiyo ya kutoa mafunzo kwa madereva na
makondakta wao itafanyika Jumamosi, Machi 22, hivyo hawatakuwa barabarani kutoa
huduma za usafiri.
Metro Trans ilisema itarejea barabarani Jumapili na Machi 23
kuendelea na hukuma kwa watumizi wa usafiri wa umma.
“Ili kuendelea kukuhudumia vyema zaidi, tumepanga programu ya uhamasishaji kwa madereva, makondakta na wafanyakazi wetu siku ya Jumamosi, tarehe 22 Machi 2025. Kwa sababu hiyo, huduma zetu zote zitasitishwa siku hii. Tutarejelea shughuli za kawaida Jumapili, tarehe 23 Machi 2025. Tunaomba radhi kwa usumbufu wowote utakaosababisha na tunathamini usaidizi wako unaoendelea,” taarifa ilisema.
Metro Trans inachukua hatua ya kutoa mafunzo upya kwa
madereva na makondakta wake ili kuzuia hali sawa na ile iliyowakuta wenzao wa
Super Metro waliopigwa marufuku kuhudumu barabarani na mamlaka ya NTSA.
Mapema Alhamisi, NTSA ilitaarifu umma kwamba sacco ya Super
Metro imepigwa marufuku kuhudumu barabarani katika kile walisema kwamba magari
mengi ya sacco hiyo yamekiuka masharti ya kuhudumu.
NTSA ilitahadharisha umma dhidi ya kuabiri magari ya sacco
hiyo na kutoa angalizo kwa maafisa wa Trafiki kuyazuia magari ya sacco hiyo
yatakayokiuka marufuku hiyo.
“Hii
ni kuufahamisha Umma kwamba Mamlaka imesimamisha leseni ya waendeshaji wa Super
Metro Limited hadi Kampuni itii kikamilifu Kanuni za Magari ya Utumishi wa
Umma, 2014 na masharti mengine yaliyowekwa,” sehemu ya chapisho hilo ilisema.
“Wananchi wametahadharishwa dhidi ya kupanda gari la kampuni ya Super Metro Limited. Idara ya Trafiki inahitajika kukamata magari ya Kampuni ambayo yatapatikana yakifanya kazi kinyume na kusimamishwa,” tangazo hilo lilisomeka zaidi.