
Mchekeshaji
mashuhuri Vincent Mwasia Mutua, maarufu kama Chipukeezy, amezungumza kwa mara
ya kwanza tangu kuteuliwa kuwa Naibu Mkurugenzi wa Itifaki na Matukio katika
Ofisi ya Rais siku ya Jumatano.
Katika ujumbe wake, Chipukeezy alieleza furaha na shukrani zake kwa nafasi hiyo, akisisitiza kuwa yuko tayari kuhudumu kwa bidii.
"Naibu Mkurugenzi wa Itifaki na Matukio, Ofisi ya Rais: Nimejawa na unyenyekevu na niko tayari kuhudumu. Wakati ukiwadia, Mungu hufanikisha. Asante, Mheshimiwa Rais @williamsamoeiruto 🙏," Chipukeezy aliandika Jumatano kwenye mtandao wa Instagram.
Habari za uteuzi wake zilifichulia na Mkuu wa Miradi Maalum ya Rais na Uratibu wa Uchumi wa Ubunifu, Dennis Itumbi, ambaye alimpongeza kwa hatua hiyo mpya.
"Hongera kwa kuteuliwa kama Naibu Mkurugenzi wa Itifaki na Matukio katika Ofisi ya Rais! Habakkuk 2:3. Nakutakia utumishi wa bidii na ari kubwa tunaposhirikiana kuendeleza Uchumi wa Ubunifu," aliandika Itumbi.
Chipukeezy ni mmoja wa wachekeshaji waliofanikiwa zaidi nchini Kenya, akiwa maarufu kwa lafudhi yake ya Kikamba na ucheshi wa kipekee. Umahiri wake ulianza kuonekana kwenye Churchill Show, jukwaa lililompa nafasi ya kung'aa na kufungua milango ya fursa nyingi, ikiwemo kuwa MC wa hafla mbalimbali za kitaifa.
Hii
si mara ya kwanza kwa Chipukeezy kushika wadhifa wa serikali. Mnamo 2018,
aliteuliwa na Rais Mstaafu Uhuru Kenyatta kuwa mjumbe wa bodi ya Mamlaka ya
Kitaifa ya Kudhibiti Matumizi ya Pombe na Dawa za Kulevya (NACADA), ambapo
alitumia nafasi hiyo kuhamasisha vijana kuhusu madhara ya dawa za kulevya.
Chipukeezy alizaliwa na kukulia Tala, Kaunti ya Machakos. Alisomea katika Shule ya Msingi ya Kwatombe kabla ya kujiunga na shule za upili za Masii na Tala. Kipaji chake cha ucheshi kilianza kuonekana akiwa shuleni, aliposhiriki katika klabu ya drama, na baadaye akajiunga na vikundi vya sanaa vilivyocheza tamthilia kwa wanafunzi wa sekondari.
Kwa juhudi zake, alipata nafasi katika Heartstrings Kenya, kundi maarufu la uigizaji, kabla ya kujiunga na East African School of Media Studies kwa masomo ya uanahabari.
Pongezi Kutoka kwa Viongozi na Wadau wa Sanaa
Uteuzi wa Chipukeezy umeibua wimbi la pongezi kutoka kwa viongozi wa serikali na wadau wa tasnia ya ubunifu.
Waziri wa Utalii na Wanyamapori, Alfred Mutua, naye alimpongeza akisema: “Ni hatua kubwa kwa sekta ya ubunifu kuona mmoja wetu akipewa nafasi ya kushiriki katika shughuli za kitaifa. Tunakutakia mafanikio tele.”
Mchekeshaji mwenzake, Daniel Ndambuki ‘Churchill’, alionyesha furaha yake kwa kusema: “Chipukeezy ameonyesha kuwa kazi ya sanaa inaweza kukupeleka mbali. Huu ni ushindi kwa wasanii wote wa Kenya.”
Mashabiki wake pia walimiminika mitandaoni wakimpongeza na kumtakia kila la heri katika majukumu yake mapya.
Kwa uteuzi huu, Chipukeezy anapata fursa ya kutumia ubunifu wake si tu katika itifaki na matukio rasmi, bali pia kusaidia kuinua sekta ya sanaa na burudani nchini Kenya.