
MSANII anayejitaja kama Tajiri zaidi katika sekta ya sanaa ya humu nchini, KRG the Don ametangaza kwamba huenda akajitosa katika sasa kuelekea uchaguzi mkuu ujao 2027.
Katika mazungumzo na YouTuber Trudy
Kitui, KRG alisema kwamba amechukua muda wake kuangalia jinsi siasa za taifa
hili zinavyoendeshwa na ameridhika kwamba amekua kuingia katika dimbwi hilo.
Aliweka wazi kwamba wakati ataingia katika
siasa, atawania ubunge japo hakusema ni eneo bunge lipi atalenga kuwakilisha
bungeni baada ya Agosti 2027.
Mkwasi huyo alisema kwamba anajua fika
siasa zinahitaji ukakamavu wa hali ya juu na kusema kwa jinsi amefuatilia
siasa, anahisi kabisa mwili na akili zake ziko tayari kuwatumikia wananchi
katika jumba la kutengeneza sheria.
“Nataka kugombea ubunge, lakini kwa sasa,
sijaanza siasa tendaji. Siasa inachukua nguvu nyingi, na zaidi ya hayo, inadai
kuwa wewe mwenyewe na kuelewa kile ambacho watu wanapitia. Nimechukua muda
kujifunza mambo hayo, na niko tayari," KRG alijieleza.
Msanii huyo ambaye alipigwa vita vya
mtandaoni na vijana wa Gen Z kutokana na misimamo yake mikali ya kusimama na
rais Ruto wakati wengi walionekana kujitenga naye alitetea ukuruba huo akisema
kwamba bado anaamini rais ndiye chaguo bora kwa taifa.
Kuhusu ni kwa nini hajateuliwa kwa
wadhifa wowote serikalini licha ya kuitetea kwa udi na uvumba wakati asilimia
kubwa ya vijana walionekana kuipinga kwenye maandamano, KRG alisema kwamba bado
anasubiri na ana Imani siku yake inakuja.
Alieleza kwamba anajua uwezo wake katika
kutekeleza majukumu mbalimbali na pengine jina lake litakapomfikia rais na amteua,
atafanya kazi kwa ufasaha.
“Watu wengi walitarajia ningepewa
wadhifa fulani, lakini unajua rais ndiye bosi na ndiye anayetathmini na kuona
ni nani ana uwezo. Pengine jina langu bado halijafika kwenye orodha, lakini
ikiwa atanipa nafasi ya kutumikia umma na nikapata nafasi hiyo, sijali. Najua
ninaweza kufanya vizuri zaidi katika kazi kama hiyo,”
alisema.
Mwaka jana baada ya kupapurana na watu
mitandaoni, KRG alitangaza kuachana na kazi ya muziki kwa kile alichokitaja
kuwa ni kupata muda zaidi wa kuzingatia biashara zake mbali na sanaa ya
burudani.